*Yatakiwa kushirikisha wananchi kikamilifu, kuhakikisha mizinga inatunzwa
Katika kuazimisha Siku ya Nyuki Duniani Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania - TFS imezindua kampeni ya utundikaji wa mizinga ya nyuki katika Msitu wa chanzo cha maji Manga uliopo Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi.
Akizindua kamapeni hio Mei 20, 2022 Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko anasema zoezi hilo la kutundika mizinga litaaendela kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini na kuitaka Wizara, TFS na wale wote wanaohusika ikiwemo Serikali Kuu ngazi ya wilaya kuhakikisha mizinga yote iliyotundikwa na ile itakayoendelea kutundikwa inatunzwa na elimu inatolewa.
“Mmenieleza kuwa jumla ya mizinga 27,600 itakwenda kutundikwa kwenye eneo hili, sasa mizinga hiyo yote itunzwe, wananchi washirikishwe kikamilifu na waendelee kupata elimu ya uhifadhi na umuhimu wa mdudu nyuki kwenye maisha ya mwanadamu, naamini wakipata elimu hata kwenye mashamba kule, wataweza kutoa maeneo yao wakapanda miti na baadaye wakatundika mizinga ili waweze kupata manufaa,
“kwa kufanya hivyo tunakuwa tumekuza uchumi, tumekuza biashara, tumejitibu, tumepata chakula kupitia uchavushaji lakini kikubwa zaidi tumetunza mazingira, na hivyo kuendelea kupata mvua za kutosha na mzunguko wetu binadamu, wanyama na viumbe wengine utaendelea kuwepo,” anasema Mh. Mrindoko.
Anaongeza kuwa nyuki ni mdudu muhimu sana kwenye Maisha ya binadamu kutokana na mdudu huyo kumuwezesha mwanadamu kupata chakula kupitia uchavushaji anaofanya kwenye mazao lakini pia mazao yake yana faida kubwa ikiwemo chakula na dawa na hivyo kuhimiza wananchi kutunza mazinzira ili mdudu huyo aweze kuishi.
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi Prof.Dos Santos Silayo Mhifadhi wa Kanda Maalumu ya Katavi Baraka Abdallah anasema katika uzinduzi huo jumla ya mizinga 40 itatundikwa kwenye eneo hilo wakati TFS ikiendelea kuweka mpango utakaowezesha kuongezeka kwa mizinga hadi kufikia mizinga isiyopungua 270 ifikapo mwishoni mwa mwaka 2023.
Mhifadhi huyo anasema walichagua eneo hili kutokana na kuwa na miti mizuri ya miombo ambayo maua yake ni chakula cha nyuki, lakini pia eneo hili lina umuhimu mkubwa kutokana na kuwa ni chanzo cha maji ambayo yanatumika na Wananchi wa Manispaa ya Mpanda na maeneo jirani.
“Msitu huu una chanzo cha maji kinachozalisha takribani mita za ujazo 1500 kwa siku na uzalishaji huo unatarajiwa kuongezeka na kufikia mita za ujazo 3000 kwa siku endapo ulinzi utaimarika. Hivyo kuna umuhimu wa kuongeza juhudi za kuutunza, na ndio mana tukaamua tuanzishe shamba darasa ili wananchi waweze kufika na kupata elimu ya shughuli rafiki wa Mazingira. Hivyo kupunguza uharibifu wa mazingira, kujiongezea kipato sambamba na kusimamia uhai wa chanzo hiki cha maji,” anasema mhifadhi huyo.
Awali akimkaribishwa mkuu wa mkoa, Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki Wizara ya Maliasili na Utalii Dr.Ezekiel Mwakalukwa alisema tukio hilo la utundikaji wa mizinga ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani nchini ikiwa na lengo la kuhamasisha jamii kufuga nyuki kwa kutumia mizinga ya kisasa ili kuzalisha asali bora inayokidhi ubora wa soko la ndani na nje.
Msitu wa chanzo cha maji Manga una ukubwa wa eneo la hekta 2300, Msitu huu awali ulikuwa ni eneo la msitu wa North East Mpanda lakini kutokana na mapitio mapya ya mpaka eneo hili lilitolewa kuwa msitu wa hifadhi ya chanzo cha maji Manga. Kwa sasa, eneo hili linasimamiwa na Bonde la Maji Ziwa Rukwa kwa kushirikiana na TFS, Vijiji vya Manga, Kasokola na Kanoge A.
Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Ufugaji wa Nyuki Daniel Chongolo akimuelekeza namna ya kuambika mzinga wa nyuki na nta Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko wakati wa zoezi la kutundika mizinga lengo likiwa ni kulivutia kundi la nyuki kuingia katika mzinga huo.
Toa Maoni Yako:
0 comments: