Mradi wa AgResults Tanzania Dairy Productivity Challenge _ ‘AgResults’, umeandaa hafla ya kutoa Tuzo ya zawadi za motisha kwa wauzaji wa pembejeo za kilimo na huduma za ugani kwa wafugaji wadogo waliochaguliwa katika awamu ya pili ya mradi. Tangu mwaka wa 2020, mradi umeshughulikia masuala ya kuongeza uzalishaji wa maziwa kwa wafugaji wadogo, kuwezesha upatikanaji wa pembejeo kwa wafugaji wadogo na kutoa zawadi za motisha kwa wafanyabiashara wanaosambaza aina mbalimbali za pembejeo kwa mfumo wa kifurushi na kutoa huduma za ugani.

Hafla hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, iliwakutanisha pamoja Wawakilishi kutoka serikalini, Washirika wa Maendeleo na wadau kutoka Sekta Binafsi kwa ajili ya kupata uelewa juu ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika awamu ya pili ya mradi na kutathimini uwezo wake wa kuimarisha sekta ya maziwa. Tukio hilo lilihusisha kupata mawasilisho mbalimbali kupitia hotuba kutoka kwa wafadhili, taasisi inayosimamia mradi ya Land O’Lakes Venture37 na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mh. Mashimba Ndaki, ambaye alihitimisha kwa kuwazawadia washindi.

Akiongea katika hafla hiyo Mkuu wa taasisi ya Land O'Lakes Venture37 John Ellenberger, alisema mradi unaendeshwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali ikiwemo Serikali ya Tanzania, kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo na kuboresha utoaji wa huduma . "Ushirikiano huu madhubuti umesababisha mafanikio tunayoyaona leo, hongera sana washindani kwa ubunifu wenu na ustahimilivu.” alisema.

Kwa upande wake,Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Mashimba Ndaki, ambaye alikuwa ni Mgeni Rasmi alisema Serikali inatambua umuhimu wa shindano hilo la kutoa zawadi kwa jinsi linavyofanikisha ukuzaji wa masoko na kunufaisha wafugaji.

“Serikali inatambua Mradi wa AgResults, kwa jinsi unavyochangia katika utekelezaji wa Mpango wa kuendeleza sekta ya Mifugo Tanzania. Hii inatupa imani kwamba kupitia ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, tunaweza kutatua changamoto nyingi zinazoikabili sekta ya mifugo nchini Tanzania." Alisema Mh.Ndaki.

Naye Rodrigo Ortiz, kutoka Sekretarieti ya AgResults, alieleza kuwa mradi umejikita kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa kupitia ubunifu wa mpango wa kutoa motisha ya zawadi ya fedha ili kushirikisha sekta binafsi kwa lengo la kunufaisha mnyororo mzima wa thamani.

“Awamu ya pili umepata mafanikio kutokana na majaribio na ubunifu katika mauzo ya awamu ya kwanza. Tumefurahishwa sana na mafanikio ya washindani na jinsi wanavyoendelea kuwekeza muda na rasilimali,kubuni mbinu mpya za kuwafikia wakulima na kuwawezesha kupata pembejeo muhimu na huduma za ugani” alisema Ortiz.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Mradi, Bi. Neema Mrema, alitoa muhtasari wa mradi na matokeo yake, akizungumzia juhudi za washindani katika kipindi cha mauzo. "AgResults imeandaa hafla hii ili kutambua juhudi za kila mshindani na kuwakabidhi zawadi zao, ambazo ili kukidhi vigezo vya kuzipata kunahitajika ubunifu mkubwa, kujifunza na kubadilika, mmekuwa mfano mzuri kwa washindani wa baadaye wa mradi huu.”alisema Mrema.

Katibu wa Ukuzaji Masuala ya Maendeleo kutoka taasisi ya Global Affairs ya nchini Canada, Christopher Duguid,alizungumzia faida za mfumo wa mashindano ya zawadi ya Lipa-kwa-Matokeo kama mbinu ya kuendeleza mifumo ya soko na kuimarisha uhusiano kati ya watendaji wa mnyororo wa thamani..

"Tunapoangazia hatua hii ambayo ni nusu ya shindano, tayari tunaweza kuona uwezekano wake wa kuongeza ufikiaji wa watu walio katika mazingira magumu na kuboresha maisha ya wafugaji wadogo wa ng'ombe wa maziwa," alisema Bw. Duguid, akiwakilisha sio tu Global Affairs Canada lakini pia jumuiya pana ya wafadhili. . "Jumuiya ya wafadhili inafurahi sana kuona kile ambacho shindano hilo litafanikisha katika miaka miwili ijayo."alisema Duguid.

Washindani kumi kati ya washiriki kumi na moja walitambuliwa kwa mauzo ya vifurushi vya pembejeo kwa wafugaji wadogo kuanzia Juni 2021 - Februari 2022 na kutunikiwa zawadi. Washindi hao ni Agricare Enterprises, ATOZ Universal Ltd, Damian Agrovet, IDD Agrovet, Kile Agrovet, Kilosa Veterinary Centre, MiL Animal Nutrition Innovation Center Ltd, Oiso Agrovet, Twins Agrovet and General Supplies, na Vetfarm. Washindi walishirikisha wakulima wadogo 8,041, na kusambaza vifurushi vya pembejeo 37,391 na kushinda jumla ya $348,283.

Mradi wa Tanzania Dairy Productivity Challenge, ni sehemu ya AgResults, inayohusisha mpango wa ushirikiano wa dola milioni 152 kati ya Serikali za Australia, Canada, Uingereza, Marekani, Bill & Melinda Gates Foundation, na Benki ya Dunia unaotumia mashindano ya zawadi kutoa motisha sekta binafsi ili kuondokana na vikwazo vya soko na kuleta mabadiliko ya kudumu. Chini ya mpango wa Lipa-kwa-Matokeo wa AgResults, mashindano haya huwahimiza watendaji kufikia viwango vya juu vya matokeo vilivyoamuliwa mapema na ubora kwa kutunukiwa tuzo za motisha za fedha.
Msimamizi wa mradi wa AgResults, Neema Mrema, akiongea wakati wa hafla hiyo.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mh. Mashimba Ndaki, akiongea wakati wa hafla hiyo iliyofanyika katika hoteli ya Hyatt Kilimanjaro jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mh.Mashimba Ndaki akimkabidhi tuzo kwa mmoja wa washindi, Mkurugenzi wa Kilosa Vetinary Centre, Dkt . Yuda Mgeni ,wakati wa hafla hiyo.Kulia ni Msajili wa bodi ya maziwa Tanzania Dkt.George Msalya. Wengine kutoka kushoto ni Msimamizi wa mradi wa AgResults nchini, Neema Mrema, na Katibu wa Ukuzaji Masuala ya Maendeleo kutoka taasisi ya Global Affairs ya nchini Canada, Christopher Duguid.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mh.Mashimba Ndaki (wa pili kulia)akikabidhi tuzo kwa kundi la VetFarm, wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo hizo uliofanyika jijini Dar es Salaam. Kulia ni Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania Dkt. George Msalya.
Washindi wa tuzo wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni Rasmi, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mh.Mashimba Ndaki (katikati waliokaa) na Msimamizi wa Mradi,Neema Mrema, Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania Dkt. George Msalya na Katibu wa Ukuzaji Masuala ya Maendeleo kutoka taasisi ya Global Affairs ya nchini Canada, Christopher Duguid
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: