Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Anamringi Macha akizungumza wakati akifungua Warsha ya 'CRDB Malkia'
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Benki ya CRDB imeendesha Warsha ya CRDB Malkia iliyokutanisha pamoja Wanawake Wafanyabiashara zaidi ya 250 Wilaya ya Kahama kwa ajili ya Kutambulisha bidhaa za Malkia ambazo ni mahususi kwa mwanamke kwa ajili ya kutoa suluhu ya changamoto zote wanazozipata wanawake katika kufikia huduma za kibenki hususani kupata mitaji na kujiwekea akiba kwa njia rafiki.
Warsha hiyo yenye lengo la kutoa mwanga mpya katika jitihada za kumkomboa na kumuwezesha mwanamke wa Kitanzania kiuchumi na kijamii imefanyika leo Jumamosi Desemba 19,2020 katika Ukumbi wa Nitesh Mjini Kahama ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Mkuu wa wilaya ya Kahama Mhe. Anamringi Macha.
Akifungua Warsha ya CRDB Malkia, Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Anamringi Macha ameipongeza Benki ya CRDB kuwa Benki ya Kizalendo iliyo mstari wa mbele kuwawezesha wanawake wa kitanzania lakini pia kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya tano kuwainua kiuchumi wanawake.
Macha alisema utafiti unaonesha biashara zinazomilikiwa na wanawake ni ndogo na zenye ukuaji hafifu akibainisha kuwa wanawake wengi wamekuwa wakikosa fursa muhimu za kujikuza kiuchumi kwa sababu mbalimbali ikiwemo mila na desturi zenye kuwatenga na ufahamu mdogo wa masuala ya fedha na uwekezaji.
“Tafiti zinaonesha licha ya kuwepo wanawake wengi wanaojishughulisha kiuchumi wengi hawatumii huduma za kibenki hasa kukopa na kuweka akiba. Zaidi ya asilimia 80% wanatumia kukopa fedha kwenye mifumo na taasisi zisizo rasmi matokeo yake biashara hazikui kwa kasi inayotakiwa kutokana na riba kubwa zinazotozwa na taasisi hizo zinazotoa mikopo umiza”,alisema Macha.
Alisema taasisi za Kifedha kama Benki ya CRDB zina jukumu la kutoa elimu juu ya huduma mbalimbali zinazotolewa kwa ajili ya kuwawezesha wanawake lakini pia kubuni bidhaa rafiki zinazoendana na mahitaji ya wanawake na zitakazosaidia kujumuisha wanawake wengi zaidi katika mfumo wa fedha.
Mkuu huyo wa wilaya ya Kahama aliwasihi wanawake wote wilayani Kahama kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa za uwezeshaji zinazotolewa na Benki ya CRDB kupitia ‘CRDB Malkia’ na wajiunge katika umoja ulioanzishwa na Benki ya CRDB ‘Malkia Business Club’.
“Naomba kutoa rai kwa Benki ya CRDB kufikisha elimu juu ya huduma za CRDB Malkia kwa wanawake wote Tanzania,mijini na vijijini. Wanawake wamekuwa wakiachwa nyuma kidogo,niwaombe muandae warsha na fursa hizi za uwezeshaji wanawake ziwafikie na wao pia”,aliongeza Macha.
Macha alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wanawake kuepuka kutumia fedha za mikopo kwa mambo ambayo hawakupanga kuyafanya huku akiwataka watu wanaotoa mikopo kwa njia zisizo rasmi kuacha mara moja kwani ni taasisi za kifedha pekee ndiyo zinaruhusiwa kutoa huduma ya mikopo.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi, Jumanne Wagana amesema Benki ya CRDB imeanzisha akaunti maalumu ya wanawake inayoitwa Malkia ambapo zaidi ya wanawake 25,000 nchi nzima wanatumia akaunti hiyo na kujiwekea malengo sambamba na mikopo ya uwezeshaji wanawake wafanyabiashara (WAFI) ambapo tayari benki imeshatoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 500.
Alisema Benki ya CRDB imekuwa ikiwapeleka wanawake wajasiriamali katika mafunzo na maonesho ndani na nje ya nchi ili kupata uzoefu na kujifunza kwa vitendo.
Pia Wagana aliwasisitiza wanawake hao kuendelea kujiwekea akiba kwenye akaunti zao ili waweze kuibuka washindi wa kampeni ya JIPE 5 inayomuwezesha mmliki wa akaunti ya CRDB Kujishindia pesa pindi akiweka pesa katika akaunti yake kupitia tawi, wakala au kwa njia ya simu.
Akitoa mada kuhusu CRDB Malkia, Meneja Uwezeshaji Wanawake Benki ya CRDB, Rachel Senni amesema wanawake ni wafanyabiashara wazuri hivyo kupitia Akaunti ya Malkia inayofunguliwa kwa shilingi 5000/= tu na haina makato kwa mwezi na unawekewa faida kila mwaka kulingana na pesa ulizoweka kwenye akaunti.
“Hii ni akaunti ya malengo binafsi na familia yako ambapo unaweza kuweka kuanzia shilingi 1,700/= na akaunti yako ikifikisha shilingi 100,000/= unaanza kuwekewa faida. Inasaidia kufikia malengo binafsi au ya familia lakini pia Bidhaa za Malkia zinakuwezesha kupata huduma za kifedha kwa urahisi zaidi, kurasimisha biashara”,aliongeza Senni.
Alifafanua kuwa lengo la CRDB Malkia ni kuleta uwiano kiuchumi kati ya wanawake na wanaume ili kufikia usawa wa kiuchumi na kwamba Benki ya CRDB imeleta mpango wa Malkia kwa sababu inamjali mwanamke na inaonesha kwa vitendo kuwa kuwa mwanamke ni wa thamani.
Pia alisema Benki ya CRDB itazindua mfumo utakaoendelea kuwaweka wanawake pamoja ‘Networking’ ili kuwa na mwendelezo wa ufuatiliaji na mafanikio ya shughuli zao.
Kwa upande wa wanawake walionufaika na mikopo ya Benki ya CRDB akiwemo Aisha Salum, Rehema Maharage na Kakusima Alex aliwataka wanawake wanaokopa fedha benki kutumia fedha walizokopa kwa shughuli walizopanga kufanya ili kupata mafanikio na si vinginevyo.
“Pesa ya mkopo siyo ya kwenda kushonea sare. Pesa ya mkopo ifanye kazi uliyoiombea,angalia kazi unayotaka,usibadili matumizi ya biashara au kazi uliyopanga kufanya ili ufanikiwe. Pesa unayokopa itumie kwa kazi unayoielewa vinginevyo utakwama”,alisema Rehema Maharage ambaye amekuwa mateja wa Benki ya CRDB tangu mwaka 2004.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Anamringi Macha akizungumza wakati akifungua Warsha ya 'CRDB Malkia' iliyokutanisha pamoja Wanawake Wafanyabiashara Wilaya ya Kahama iliyoandaliwa na Benki ya CRDB katika Ukumbi wa Nitesh Hotel Mjini Kahama leo Jumamosi Desemba 19,2020. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Anamringi Macha akizungumza wakati akifungua Warsha ya 'CRDB Malkia' iliyokutanisha pamoja Wanawake Wafanyabiashara Wilaya ya Kahama iliyoandaliwa na Benki ya CRDB.
Kaimu Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi, Jumanne Wagana akizungumza kwenye Warsha ya 'CRDB Malkia' iliyokutanisha pamoja Wanawake Wafanyabiashara Wilaya ya Kahama iliyoandaliwa na Benki ya CRDB.
Kaimu Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi, Jumanne Wagana akielezea kuhusu akaunti za watoto Junior Jumbo,Scholar Account, Bima ya majanga mbalimbali zinazotolewa na Benki ya CRDB.
Meneja Uwezeshaji Wanawake Benki ya CRDB, Rachel Senni akizungumza kwenye Warsha ya 'CRDB Malkia' iliyokutanisha pamoja Wanawake Wafanyabiashara Wilaya ya Kahama iliyoandaliwa na Benki ya CRDB.
Mnufaika wa Mikopo ya Benki ya CRDB Rehema Maharage akizungumza kwenye Warsha ya 'CRDB Malkia' iliyokutanisha pamoja Wanawake Wafanyabiashara Wilaya ya Kahama iliyoandaliwa na Benki ya CRDB.
Mnufaika wa Mikopo ya Benki ya CRDB, Aisha Salum akizungumza kwenye Warsha ya 'CRDB Malkia' iliyokutanisha pamoja Wanawake Wafanyabiashara Wilaya ya Kahama iliyoandaliwa na Benki ya CRDB.
Mnufaika wa Mikopo ya Benki ya CRDB, Kakusima Alex akizungumza kwenye Warsha ya 'CRDB Malkia' iliyokutanisha pamoja Wanawake Wafanyabiashara Wilaya ya Kahama iliyoandaliwa na Benki ya CRDB.
Wanawake wafanyabiashara wilayani Kahama wakiwa katika Warsha ya CRDB Malkia
Afisa wa Benki ya CRDB, Nazir Bakari akiendelea na zoezi la kufungua Akaunti ya Malkia mmoja wa wafanyabiashara wilayani Kahama.
Afisa wa Benki ya CRDB Saumu Bakari akiendelea na zoezi la kuwafungulia akaunti ya Malkia
Wanawake wafanyabiashara wilayani Kahama wakiwa katika Warsha ya CRDB Malkia
Maafisa wa Benki ya CRDB na Wanawake wafanyabiashara wilayani Kahama wakiwa katika picha ya pamoja baada ya warsha ya CRDB Malkia Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Toa Maoni Yako:
0 comments: