Na John Mapepele.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ametoa siku saba kwa makatibu wakuu wa Kilimo na Mifugo kuwasilisha wizarani kwake taarifa ya kwanini bei ya mbegu za mahindi na mtama pamoja na gharama za uhimilishaji mifugo nchini ni kubwa licha ya uwepo wa usimamizi wa Serikali,pia kuendelea kuagiza mbegu za matunda na mbogamboga nje ya nchi ambazo zinaweza kuzalishwa hapa nchini.
Mbali na hilo, Waziri Mpina pia amezitaka Taasisi za TPRI,TFDA,TBS na Kurugenzi ya Huduma za Mifugo katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi kujitathmini upya utendaji kazi wao kama wanastahili kuwepo baada ya kushamiri kwa dawa na viuatilifu vya kilimo na mifugo feki na vilivyokwisha muda wa matumizi na kusababisha hasara kubwa kwa wakulima,wafugaji na Taifa kwa ujumla.
Akifungua maonesho ya Kilimo Nane Nane, Kanda ya Kaskazini yanayofanyika katika viwanja vya Themi jijini Arusha, Waziri Mpina alisema ni jambo la aibu kwa viongozi kuendelea kuwakutanisha wakulima na wafugaji katika maonesho hayo kila mwaka huku changamoto zao za msingi ikiwemo kuuziwa mbegu kwa bei kubwa, dawa na viuatilifu visizoua wadudu kwenye mazao na mifugo yao zikiwa hazijapatiwa ufumbuzi.
Alisema baadhi ya wazalishaji wa mbegu za kilimo nchini wamekuwa wakiuza kwa bei kubwa kiasi cha kuwakatisha tamaa wakulima kutumia mbegu bora ambapo baadhi ya kampuni zimekuwa zikiuza kilo moja ya mbegu ya mahindi kwa sh. 6,000 wakati bei wanayonunua kwa wakulima wa kilimo cha mkataba cha uzalishaji mbegu kwa kilo ni sh 1,200 na bei ya mahindi ya kawaida kwa kilo ni sh. 600 tu.
Pia gharama za uhamilishaji mifugo nchini dozi moja huuzwa wastani wa sh 3,000 kutoka katika vituo vya Taifa vya uhamilishaji mifugo lakini kampuni binafsi za uhamilishaji huwatoza wafugaji wastani wa sh 20,000 hadi sh 40,000 kwa dozi, gharama ambazo wafugaji wengi hawawezi kuzimudu.
Pia Waziri Mpina aliagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinakuwa na shamba darasa la bwawa la ufugaji wa samaki ili kuongeza upatikanaji wa chakula na biashara yamazao ya uvuvi, ajira na mapato ya Serikali.
Kuhusu sekta ya mifugo Waziri Mpina alisema licha ya mikoa hiyo ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara kuwa na takribani asilimia 15 ya mifugo yote nchini lakini hakuna kiwanda hata kimoja cha kuchakata mazao ya mifugo hali ambayo inasababisha mifugo mingi kutoroshwa nchi jirani ya Kenya ajili ya kutafuta masoko.
Pia aliagiza halmashauri zote nchini kufanyia matengenezo na ukarabati minada,machinjio na majosho ili kuongeza tija katika uzalishaji na ukusanyaji maduhuli yatokanayo na sekta ya mifugo
Kuhusu maendeleo ya sekta ya uvuvi, Waziri Mpina alisema kanda ya kaskazini inayo fursa kubwa ya uvuvi katika Ziwa Eyasi, Duluti, Manyara, Babati,Buruge, Bassotu, Jipe, Chala na Karamba na katika Bwawa la Nyumbaya Mungu, Kalemawe na mabwawa ya kuchimba ambapo aliagiza kufanyika kwa uvuvi endelevu na kuachana na uvuvi haramu.
Serikali pia inakusudia kukiboresha zaidi kituo cha kuzalisha vifaranga vya samaki Tanga ili kiweze kuchochea ufugaji samaki kwenye mabwawa katika kanda hiyo.
Alisema ni jambo la aibu Taifa kuendelea kutumia mabilioni ya fedha kuagiza samaki kutoka nje ya nchi wakati fursa kubwa za uwekezaji kwenye sekta hiyo zipo hapa nchini na kwamba Serikali ya awamu ya tano imejipanga kuhakikisha uzalishaji wa samaki nchini unaongezeka.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega alisema kanda ya kaskazini ina jumla ya ng’ombe milioni 4.4, Mbuzi milioni 4.1, Kondoo milioni 2.7 na kwamba bado haijaweza kunufaisha vya kutosha kanda hiyo na kuahidi kusimamia kikamilifu maagizo mapya ya Waziri Mpina ili kuhakikisha sekta za Kilimo na Mifugo zinatoa mchango unaostahili kwa maendeleo ya kanda hiyo na Taifa kwa ujumla.
Toa Maoni Yako:
0 comments: