Hussein Makame-NEC
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Dkt. Athumani Kihamia amesema Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Buyungu ataendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuwa malalamiko yaliyotolewa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ya kumkataa msimamizi huyo hayakufuata taratibu za kisheria.
Akitoa ufafanuzi huo jijini Dar es Salaam leo, Dkt. Kihamia alisema kuwa kwa mujibu wa Kifungu cha 7 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343, malalamiko hayo hayana msingi wa kisheria kwa sababu hayakuja kama rufaa ila yametolewa kama malalamiko.
“Kwa maana hiyo napenda kuwajulisha umma kwamba malalamiko haya hayamuondolei sifa Msimamizi wa Uchaguzi kwa kumuondoa kusimamia shughuli za Uchaguzi katika Jimbo la Buyungu” alisema Dkt. Kihamia na kuongeza:
“Kwa kuwa Chadema kimelalamika kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na malalamiko hayo wameyaleta kama barua, kwa kuwa kuna Kamati ya Maadili ngazi ya Taifa, malalamiko hayo yalipaswa yaletwe ndani ya muda unaokubalika ambayo ni saa 48 tangu kupokea hizo taarifa’.
Alisema majibu haya yametokana kwa jinsi Tume ilivyochunguza upande unaolalamikiwa na kujiridhisha ingawa, alisema Tume itaendelea kufuatilia kwa karibu kuona kila kitu kinakwenda vizuri na kwamba hakuna jambo linaloweza kuharibu Uchaguzi.
Dkt. Kihamia alikihasa Chadema kuwa kama kuna kasoro zingine zozote ndogo ndogo ambazo zinaweza kutatulika kwa njia ya kawaida Tume itatekeleza majukumu yake katika kasoro hizo.
Akitaja malalamiko ya Chadema, Dkt. Kihamia alisema Chadema kupitia Katibu Mkuu wake, kiliandika barua Tume kikimlalamikia Msimamizi wa Uchaguzi kwamba ratiba ya mtiririko wa Uchaguzi haikutolewa.
“Baada ya kupokea malalamiko hayo tulijiridhisha na kugundua kuwa Msimamizi wa Uchaguzi katika Jimbo hilo alikutana na vyama tarehe 7 Julai, 2018 na vyama vilipokea ratibu ya shughuli za uchaguzi wa jimbo hilo siku hiyo na vingine vilipokea tarehe 10 Julai, 2018”, alisema Dkt. Kihamia.
Alitaja madai mingine kwamba orodha ya wasimamizi wa vituo vya kupigia kura haikutolewa, na kueleza kuwa ushahidi ilionao Tume unaonesha kuwa orodha hiyo ilitolewa tarehe 5 na 6 Julai, 2018 na siku ya mwisho ya kutoa ilikuwa tarehe 31 Julai, 2018.
“Hoja ya tatu ni kwamba viapo vya mawakala havikutolewa kwa wakati.Taarifa rasmi inaonesha viapo vilitolewa siku saba kabla ya siku ya Uchaguzi na vimezingatia matakwa ya Sheria kwa kuwa vilitolewa tarehe 5 Agosti na Uchaguzi ni tarehe 12 Agosti mwaka huu”, alibainisha Dkt. Kihamia.
Kuhusu hoja ya nne iliyotolewa na Chadema kwamba Msimamizi wa Uchaguzi hakuonesha sehemu ambapo kura zanatakiwa kujumlishwa, Dkt. Kihamia alisema uchaguzi ni Agosti 12, 2018 taarifa hiyo inakiwa kutolewa isizidi siku ya tarehe 11 Agosti, 2018 ambapo tarehe hiyo bado haijafika.
Alisema kuwa Tume inaamini kuwa muda wowote taarifa hizo zitatolewa na pia kwa kuwa haijasikia malalamiko kutoka vyama vingine tisa vinavyoshiriki uchaguzi katika jimbio la Buyungu, inawezekana Chadema mawasiliano hayakuwa mazuri ndani ya chama hicho.
Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Buyungu na kata 77 unatarajiwa kufanyika Agosti 12 mwaka huu huku Uchaguzi katika baadhi ya kata wagombea wake wakitangazwa kupata bila kupingwa.
Toa Maoni Yako:
0 comments: