Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizindua vituo 51 vya kufuatilia taarifa za hali ya hewa katika viwanja vya Ofisi ya Halmashauri ya wilaya ya Bahi mkoani Dodoma Juni 27, 2018. Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama. Wanne kushoto ni Mwakilishi Mkaazi wa Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Bibi Natalie Boucly. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama chombo cha kupima wingi wa mvua baada ya kuzindua vituo 51 vya kufuatilia taarifa za hali ya hewa katika viwanja vya Ofisi ya Halmashauri ya wilaya ya Bahi mkoani Dodoma Juni 27, 2018. Wengine pichani kutoka kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu,Jenista Mhagama,Waziri wa Maji, Mhandisi Isaack Kamwele, Mwakilishi Mkaazi wa Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Bibi Natalie Boucly na kulia ni Mbunge wa Viti Maalum kutoka mkoa wa Dodoma, Felista Bura.
Baadhi ya wananchi walioshiriki katika uzinduzi wa vituo 51 vya kufuatilia taarifa za hali ya hewa uliofanywa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika viwanja vya Ofisi ya Halmashauri ya wilaya ya Bahi mkoani Dodoma Juni 27, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akibonyeza kitufe wakati alipozindua vituo 51 vya kufuatilia taarifa za hali ya hewa katika viwanja vya Ofisi ya Halmashauri ya wilaya ya Bahi mkoani Dodoma Juni 27, 2018. Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge,Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
WAZIRIMKUU Kassim Majaliwa amewataka wataalamu wa sekta za kilimo, mifugo na maji watumie taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ili waongeze ufanisi katika utendaji kazi wao.
Ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Juni 27, 2018) wakati akizinduavituo 51 vya kufuatilia taarifa za hali ya hewa, vituo 15 vya haidrolojia, kanzidata ya taarifa za hali ya hewa na kituo cha operesheni na mawasiliano ya dharura wilayani Bahi, Dodoma.Amesemakuwa kuongezeka kwa vituo vipya vya kisasa vya ufuatiliaji wa mwenendo wa hali ya hewa kumeboresha uhakika wa utabiri kutoka asilimia 81 hadi 87 kama inavyoshuhudiwa kwenye taarifa zinazotolewa katika siku za hivi karibuni. “Hivi sasa tukiambiwa kwamba mvua itanyesha katika maeneo fulani tunakuwa na uhakika kwa asilimia 87 ya utabiri huo,”.
“Vituo hivi ni muhimu katika kuimarisha uwezo wa nchi wa utoaji wa huduma za hali ya hewa na haidrolojia kwa ajili ya shughuli za maendeleo na kuongeza ufanisi katika utoaji wa tahadhari za awali za majanga yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa na mabadiliko ya tabianchi,”. Amesema kupitia mradi huo uliofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Serikali imeweza kufungua vituo 51 vya kisasa vya hali ya hewa katika maeneo mbalimbali nchini na vituo 15 vya kupima ujazo wa maji kwenye mito iliyopo kwenye mabonde ya Pangani, Ruvuma na Pwani ya Kusini ambavyo vinajiendesha vyenyewe.
“Pia, mradi huu umeiwezesha Serikali kuanzisha kanzidata ya takwimu na taarifa za mafuriko na ukame na taarifa za hali ya hewa na kuondoa ucheleweshwaji wa kupata takwimu au taarifa kutoka Wizara moja kwenda Wizara nyingine,” amesema. Hata hivyo, Waziri Mkuu ameziagiza Wizara ya Maji na Umwagiliaji na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano zitenge fedha kwenye bajeti zao ili ziweze kufuatilia na kusimamia mradi huo baada ya wafadhili kumaliza muda wao.
Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli, itaendelea kushirikiana na washirika wa maendeleo katika kuhakikisha kuwa vituo na mifumo iliyowekwa inafanya kazi ipasavyo kwa usimamizi bora ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.Uzinduzi huo umehudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Bibi Jenista Mhagama, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe na Waziri wa Kilimo, Dkt. Charles Tizeba.
Wengine ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Kangi Lugola, Wabunge na Mwakilishi Mkaazi wa Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Bibi Natalie Boucly.
Toa Maoni Yako:
0 comments: