Kaimu Mkuu wa Idara Wateja Maalum wa Benki ya Stanbic Tanzania, Beatrice Kisoka (wa tatu kulia) akipokea tuzo ya Benki Bora ya Kimataifa kwa Wateja Maalum katika tuzo za Euromoney Private Banking Awards 2026 zilizofanyika jijini London mwishoni mwa wiki. Pichani ameambatana na viongozi wengine kutoka Benki ya Stanbic Tanzania. Benki ya Stanbic ilipata tuzo tatu katika hafla hiyo zikiwemo Benki Bora ya Kimataifa kwa Wateja Maalum, Benki Bora kwa Kizazi Kijacho, na Benki Bora kwa Huduma kwa Wateja.

Ujumbe wa Benki ya Stanbic Tanzania uliohudhuria hafla ya utoaji Tuzo za Euromoney Private Banking Awards 2026 zilizofanyika jijini London, Uingereza mwishoni mwa wiki.

Na Mwandishi Wetu.

Benki ya Stanbic Bank Tanzania imeendelea kuthibitisha ubora wake katika sekta ya fedha baada ya kutwaa tuzo tatu za kimataifa kutoka Euromoney, zikiwemo Benki Bora ya Kimataifa kwa Wateja Maalum, Benki Bora kwa Kizazi Kijacho na Benki Bora kwa Huduma kwa Wateja.

Tuzo hizo zilitangazwa katika hafla ya Euromoney Private Banking Awards 2026 iliyofanyika jijini London, kufuatia tathmini ya kina iliyofanywa na jopo huru la wataalamu wa sekta ya fedha duniani.

Mafanikio hayo yanaifanya Stanbic kuwa miongoni mwa taasisi zinazoongoza katika kutoa huduma za kifedha zilizoandaliwa mahsusi kwa wateja, huku ikitambuliwa kwa mara ya pili mfululizo kama benki bora ya kimataifa kwa wateja maalum.

Akizungumzia tuzo hizo, Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Manzi Rwegasira, alisema mafanikio hayo yanaakisi mabadiliko ya namna mali zinavyosimamiwa nchini, hasa katika mazingira ya uchumi unaokua.

“Kadri uchumi wa Tanzania unavyoendelea kukua, wateja wanahitaji mipango madhubuti ya kulinda na kurithisha mali zao kwa vizazi vijavyo. Haya ndiyo maeneo tunayoyawekea nguvu kubwa,” alisema.

Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania, uchumi wa nchi unatarajiwa kukua kwa kati ya asilimia 5 hadi 6, hali inayochochea ongezeko la ukwasi hasa kwa wajasiriamali na biashara za kifamilia.

Tuzo ya Benki Bora kwa Kizazi Kijacho imeangazia juhudi za Stanbic katika kuwaandaa vijana na warithi kusimamia mali kwa uwajibikaji, wakati tuzo ya Huduma kwa Wateja ikitambua ubora wa ushauri wa kifedha unaotolewa kwa wateja kwa kuzingatia mahitaji yao ya muda mrefu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi na Maalum, Omari Mtiga, alisema benki hiyo inalenga kujenga mahusiano ya muda mrefu na wateja wake kwa kuelewa mahitaji yao ya kifamilia na kibiashara.

Naye Kaimu Mkuu wa Idara ya Huduma kwa Wateja Maalum, Beatrice Kisoka, alibainisha kuwa wateja wengi sasa wanazingatia zaidi uendelevu wa mali zao na mchango wake kwa vizazi vijavyo.

“Wateja wanahitaji zaidi ya mafanikio ya sasa; wanataka kuona uthabiti na mwendelezo wa mali zao kwa muda mrefu,” alisema.

Mafanikio hayo yanaongezea hadhi ya benki hiyo ambayo pia ilitambuliwa kama benki bora nchini Tanzania mwaka 2025 na jarida la The Banker, hatua inayodhihirisha uthabiti wake katika kutoa huduma bora za kifedha.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: