Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

Tanzania sasa imejiweka kwenye ramani ya tiba utalii barani Afrika baada ya Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila (MNH-Mloganzila) kuzindua Kliniki Maalumu (Premier Clinic) yenye viwango vya kimataifa, faragha na teknolojia za kisasa zinazolingana na mataifa yaliyoendelea.

Akizindua kliniki hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, alisema hatua hiyo ni uthibitisho wa uwekezaji mkubwa wa Serikali ya Awamu ya Sita katika sekta ya afya, ambao umechochea ubunifu na kuifanya Tanzania kuwa kituo kipya cha matibabu ya kimataifa.

“Huduma hizi tulizozizoea kuzitafuta nje ya nchi sasa zinapatikana hapa nyumbani. Serikali imejenga misingi imara kwa kuimarisha miundombinu, kuongeza bajeti ya dawa, kusomesha wataalam na kununua vifaa tiba vya kisasa,” alisema Chalamila.

Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dkt. Delilah Kimambo, alisema Premier Clinic inalenga kuvutia wagonjwa kutoka Tanzania, Afrika Mashariki, Kati na hata nje ya bara, huku ikijikita katika misingi mitatu: ubora wa huduma, ufanisi na ubunifu.
Tunataka Watanzania na wageni waone Muhimbili siyo tu hospitali ya taifa, bali ni kitovu cha tiba cha kikanda na kimataifa,” alisema Dkt. Kim
ambo.

Naye Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya MNH, Dkt. Khadija Malima, alisisitiza kuwa bodi itaendelea kuhakikisha huduma bora zinadumu na kuimarisha imani ya wananchi na wageni kutoka nje.

Kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Mratibu wa Tiba Utalii, Dkt. Asha Mahita, alisema kuzinduliwa kwa kliniki hiyo kutasaidia Tanzania kushindana kimataifa katika sekta ya tiba utalii, kwani wagonjwa kutoka mataifa jirani na ya mbali wamekuwa wakija nchini kwa ajili ya uchunguzi na matibabu.

Uzinduzi huu unaweka Tanzania katika nafasi mpya, ambapo huduma bora za afya na faragha zinapatikana kwa viwango vya kimataifa bila kulazimika kusafiri kwenda nje ya nchi.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: