Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.
MGOMBEA wa kiti cha Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewataka wananchi kuendelea kudumisha amani akisisitiza kuwa ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa lolote.
Akizungumza katika mkutano mkubwa wa kampeni wa Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, uliofanyika katika Uwanja wa Michezo Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja, tarehe 18 Septemba 2025, Dkt. Mwinyi alisema wananchi wana kila sababu ya kuendelea kuiamini CCM kutokana na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020–2025.
Alifafanua kuwa ilani hiyo imeleta mageuzi makubwa katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi, hatua ambazo zimejibu changamoto nyingi zinazowakabili wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Dkt. Mwinyi pia aliwahimiza wanachama na wapenzi wa CCM pamoja na wananchi kwa jumla kujitokeza kwa wingi ifikapo Oktoba 29, 2025 kushiriki uchaguzi mkuu, akisema ni muhimu kuipigia kura CCM ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana na kuimarisha zaidi kasi ya maendeleo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Taifa na Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akimnadi Dkt. Mwinyi, alimuelezea kuwa kiongozi hodari, mchapakazi, msikivu na mwenye dira ya kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.
“Dkt. Mwinyi ni kiongozi sahihi wa kuendelea kuiongoza Zanzibar. Katika kipindi chake cha kwanza ameonyesha ufanisi mkubwa, hivyo anastahili kupewa kipindi cha pili ili kukamilisha ndoto za wananchi wa Zanzibar,” alisema Dkt. Samia.
Mkutano huo ulihudhuriwa na mamia ya wananchi, viongozi wa CCM, pamoja na wanachama waliokuwa wamevalia mavazi ya chama hicho huku wakishangilia kwa hamasa, ishara ya mshikamano na mshikikiano kuelekea uchaguzi mkuu.




.jpeg)
.jpeg)



.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments: