Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Arusha
Serikali imesema imekusanya taarifa za Anwani za Makazi Milioni 12.3 nchi nzima, zinazotakiwa kuhuishwa kila wakati ili ziendelee kuwa taarifa sahihi wakati wote kwa kuwa zinabadilika mara kwa mara kutokana na sababu mbalimbali.
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Nicholaus Merinyo Mkapa, tarehe 14 Agosti, 2024 wakati wa ufunguzi wa Zoezi la Uhakiki wa Taarifa za Anwani za Makazi mkoani Arusha.
Bw. Mkapa amesema, ni lazima iwepo mikakati endelevu ya kuhakikisha Mfumo wa Anwani za Makazi yaani NaPA unakuwa na taarifa sahihi kila wakati kwa kuwa nyumba mpya zinajengwa kila siku, upimaji wa viwanja unaoendelea katika maeneo mbalimbali pamoja, watu kuhama kutoka eneo moja Kwenda lingine na matumizi yanabadilika na sababu nyingine kadhaa.
“Katika kufanikisha suala hilo, wizara imeandaa mkakati wa kufanya uhakiki wa taarifa katika halmashauri zote nchini (Mass Data Cleaning), unaokwenda sambamba na kujenga uwezo kwa Waratibu, Wataalamu Wenyeviti na watendaji wa Kata na Mitaa ili waweze kuendelea kutekeleza shughuli za Mfumo wa Anwani za Makazi katika maeneo yao”, amesema Bw. Mkapa.
Naibu Katibu Mkuu huyo amesema hadi sasa, wizara imeshafanya zoezi la uhakiki na kujenga uwezo katika Halmashauri 31, kati ya hizo, 19 ni za Tanzania Bara na 11 za Tanzania Zanzibar.
Amesema, katika uhakiki huo, wizara imefanikiwa kuhuisha zaidi ya taarifa za anwani Milioni 2.3, kutoa anwani mpya zaidi ya 500,000 na kujenga uwezo kwa wataalamu, wenyeviti na watendaji wapatao 6,621.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Mawasiliano wa Wizara hiyo, Bw. Mulembwa Munaku amesema kuwa zoezi la Uhakiki linafanyika baada ya wizara kufanya tathmini na kubainisha mapungufu mbalimbali yakiwemo baadhi ya taarifa zilizokusanywa kukosa sifa, kutoa majina ya Barabara bila kuzingatia miongozo na baadhi ya wananchi kutofikiwa na zoezi.
Wenyeviti wa mitaa,watendaji wa kata na mitaa, Wakurugenzi wa halmashauri, Makatibu tawala wilaya pamoja na viongozi mbalimbali wa taasisi za umma na binafsi wakishiriki mafunzo maalum ya zoezi la Uhakiki wa Taarifa za Anwani za Makazi kutoka Mkoa wa Arusha tarehe 14 Agosti, 2024.
---
Bw. Munaku amesema ufunguzi uliofanyika leo unakwenda sambamba na Utoaji wa Mafunzo kwa washiriki ambapo Mada mbalimbali zitatolewa kama vile Utambuzi na utoaji wa majina ya barabara na namba za Anwani, Mfumo wa kidijitali wa Anwani za Makazi, kupata uelewa wa maswali yanayotumika kukusanya taarifa za Anwani na Utaratibu wa Kusajili na Kuhakiki majina wa Barabara.
Toa Maoni Yako:
0 comments: