Na Mwandishi Wetu WHMTH, Arusha

Wananchi wameombwa kutoa taarifa kuhusu uharibifu wa miundombinu ya Anwani za Makazi katika maeneo yao na kuhimizana kuilinda kwa mfumo wa ulinzi shirikishi kwani miundombinu hiyo imetengenezwa kwa gharama kubwa.

Wito huo umetolewa leo tarehe 14 Agosti, 2024 jijini Arusha na Katibu Tawala Msaidizi, Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Mkoa wa Arusha David Lyamong katika hafla ya Ufunguzi wa Zoezi la Uhakiki wa Taarifa za Anwani za Makazi mkoani humo.

Bw. Lyamong anayekaimu Nafasi ya RAS wa mkoa huo amesema, zipo taarifa kuwa katika baadhi ya maeneo, miundombinu ya Mfumo wa Anwani za Makazi ambayo ni nguzo za majina ya Barabara na vibao vya namba za Nyumba, imeanza kuharibiwa, jambo alilosema siyo zuri.
Amekumbusha kuwa “Wengi wetu tuliamini kuwa zoezi la Anwani za Makazi liliisha baada ya kufanya Sensa ya Watu na Makazi mwezi Agosti, 2022, lakini hapana, kila Mtanzania anatakiwa kufahamu kuwa utekelezaji wa zoezi hili ni endelevu, na halikuisha baada ya sensa”.

Ufunguzi wa zoezi la Uhakiki wa Taarifa za Anwani za Makazi katika Mkoa wa Arusha umefanyika kwa mara ya kwanza, ukitarajiwa kufanyika katika halmashauri sita za mkoa huo ikiwemo, Arusha Jiji, Wilaya ya Arusha, Ngorongoro, Monduli, Karatu na Longido.

Bw. Lyamong amesema, kwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kuamua kufanya hafla ya zoezi hilo kwenye Halmashauri 6 za mkoa huo kwa mara moja, ni heshima kubwa kwa kutambua mchango wa Mkoa wa Arusha katika uchumi wa nchi.
Amesema, kwa kuwa zoezi la uhakiki wa Anwani za Makazi linaambatana na mafunzo kwa wenyeviti na watendaji wa kata na mitaa wa halmashauri zote utakakofanyika uhakiki wa taarifa, ni muhimu viongozi hao wakazingatia mafunzo hayo ili wakawasaidie wakazi wa maeneo yao.

"Endapo kila jengo litasajiliwa na kuweza kuonekana na kufikika kupitia Mfumo wa Anwani za Makazi basi tutakuwa tumepiga hatua kubwa katika kuimarisha usalama ndani ya mkoa wetu wa Arusha na nchi kwa ujumla" alisisitiza Katibu Tawala huyo.

Katibu Tawala Msaidizi huyo wa Mkoa wa Arusha amesema, mkoa huo unatambua umuhimu wa Anwani za Makazi, kwani ni miongoni mwa mipango ya mkoa huo wa kuimarisha huduma za utambuzi ili kujenga mazingira rafiki na kuongeza usalama kwa watalii na wageni wanaofika jijini Arusha.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: