Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb), alipowasili katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera kwa ajili ya kuanza ziara yake ya kukagua ujenzi wa minara ya mawasiliano ya simu katika Wilaya ya Muleba na Biharamulo mkoani humo leo tarehe 16 Julai, 2024.
Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Kagera

Katika kuhakikisha Mikoa iliyo pembezoni inaungwanishwa na Tanzania ya Kidigitali, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote unatarajia kujenga minara 45 katika Kata 44 yenye thamani ya sh. Bilioni 6.6 za kitanzania katika Mkoa wa Kagera.

Hayo yamebainishwa tarehe 16 Julai, 2024 na Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Bi. Justina Mashiba, wakati akitoa taarifa ya utendaji wa Mfuko katika Mkoa wa Kagera, mbele ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb.) aliye katika siku ya pili ya ziara yake Mikoa ya Kanda ya Ziwa kukagua ujenzi wa Minara ya Mawasiliano ya simu.

Bi. Mashiba amesema minara hiyo 45 ya Kagera ni kati ya minara 758 inayofadhiliwa na Serikali kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka wa fedha 2023/2024 hadi 2024/2025 , ambapo kwa Mkoa wa Kagera ikitarajiwa kuwanufaisha Watanzania 801,961 itakapokamilika mwanzoni mwa mwaka 2025.

Amesema, Mkoa wa Kagera ni kati ya mikoa 26 Tanzania Bara, itakayonufaika na kwamba wilaya za mkoa huo inakojengwa minara 45 na idadi ya minara kuwa ni Biharamulo (13), Bukoba DC (1), Karagwe (14), Missenyi (3), Kyerwa (4), Muleba (8), na Ngara (2).

Amesema hadi kufikia mwishoni mwa Juni 2024, jumla ya minara kumi (10) imeshawashwa na Watoa Huduma za Mawasiliano.
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Bi. Justina Mashiba akitoa wasilisho la hali ya utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Minara ya Mawasiliano kwa Mkoa wa Kagera mbele ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe Nape Moses Nnauye (Mb), Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe Erasto Sima na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Kagera, Wakuu wa Taasisi na watoa huduma tarehe 16 Julai, 2024 kwenye Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa.
Mtendaji Mkuu huyo wa UCSAF amesema, kupitia minara 10 iliyowashwa vijiji kadhaa vya wilaya hizo vimenufaika na mradi huo, katika kata 44 zikiwemo Kaniha, Nyakahura, Nyantakara, Nyarubungo, Igurwa, Kihanga, Kakunyu, Karambi na Ngenge.

Kwa ujumla tangu mwaka 2009 jumla ya minara 80 imejengwa katika wilaya saba (7) za Mkoa wa Kagera, kutokana na makubaliano kati ya Serikali, kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na watoa huduma za mawasiliano.

Bi. Mashiba amesema, minara hiyo iliyojengwa kwa teknolojia ya 2G, 3G na 4G, kwa ruzuku iliyotolewa na UCSAF, imegharimu jumla ya Shilingi Bilioni 10.89, na inawanufaisha Watanzania 1,248,91

Ametaja wilaya 7 zinazofaidika na minara hiyo na idadi ya minara iliyojengwa, kwenye mabano, kuwa ni Biharamulo (15), Bukoba DC (5), Karagwe (22), Missenyi (14), Kyerwa (6), Muleba (4), na Ngara (14).
Mkurugenzi wa Leseni na Ufuatiliaji kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Wakili John Daffa akitoa wasilisho la hali ya huduma ya mawasiliano kwa Mkoa wa Kagera mbele ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe Nape Moses Nnauye (Mb), Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe Erasto Sima na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Kagera, Wakuu wa Taasisi na watoa huduma walio chini ya Wizara tarehe 16 Julai, 2024 kwenye Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: