Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Kigoma.
Watanzania wapatao 866,352, wamenufaika na huduma bora za mawasiliano katika Mkoa wa Kigoma, kutokana na mradi wa minara ya simu 47 iliyojengwa na kuanza kutumika mkoani humo.

Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Bi. Justina Mashiba, amebainisha hayo Julai 15, 2024, wakati akitoa taarifa ya utendaji wa Mfuko katika Mkoa wa Kigoma, mbele ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb.)
Bi. Mashiba amesema, minara hiyo iliyojengwa kwa teknolojia ya 2G, 3G na 4G, kwa ruzuku iliyotolewa na UCSAF, kwa makubaliano na watoa huduma, imegharimu jumla ya Shilingi za kitanzania Bilioni 6.3.

Ametaja wilaya zilizofaidika na minara hiyo na idadi ya minara iliyojengwa, kwenye mabano, kuwa ni Buhigwe (6), Kakonko (12), Kasulu DC (6), Mji wa Kasulu (5), Kibondo (8), Kigoma DC (2) na Uvinza (8).
Bi. Mashiba amesema, pia Mkoa wa Kigoma ni kati ya mikoa 26 Tanzania Bara, itakayonufaika na mradi wa minara 758 inayoendelea kujengwa nchi nzima na inayotarajiwa kuwafikia Watanzania zaidi ya milioni 8.5 itakapokamilika mwanzoni mwa mwaka 2025.

Amezitaja wilaya za Mkoa wa Kigoma inakojengwa minara hiyo na idadi ya minara kuwa ni Kasulu (3), Kibondo (3) na Uvinza (2), na kutaja ruzuku ya Serikali kupitia UCSAF iliyotumika kwa minara hiyo kuwa ni Shilingi Bilioni 1.38.
Amesema, hadi kufikia mwishoni mwa Juni 2024, jumla ya minara mitatu ya mradi hiyo imekamilika na kuwashwa, na kuvinufaisha vijiji kadhaa vikiwemo Kijiji cha Katete wilayani Uvinza, na Bunyango na Kumbanga wilayani Kibondo.

UCSAF ni taasisi ya Serikali iliyoanzishwa kwa lengo la kufikisha huduma za mawasiliano vijijini na mijini, kusiko na mvuto wa kibiashara, kwa kushirikiana watoa huduma za mawasiliano, zikiwemo kampuni za Airtel, Halotel, Tigo, TTCL na Vodacom.

Tangu ulipoanziswa mwaka 2009 hadi mwaka 2024 UCSAF imeshazifikia jumla ya Kata 1,349 ambako minara 1,481 ya mawasiliano imejengwa na kunufaisha wananchi Milioni 16.59 nchi nzima.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: