Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Abel Makubi akizungumza na wataalamu wa afya katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) baada ya kutembelea miundombinu ya kutoa huduma ikiwamo kituo cha kupandikiza ulotu kwa wagonjwa wenye saratani damu.
Baadhi ya wataalamu wa afya MNH na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) wakimsikiliza Prof. Makubi.
Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Lawrence Museru akitoa taarifa kuhusu uanzishaji wa huduma za kibingwa ikiwamo huduma ya upandikizaji uloto kwa wagonjwa wenye saratani ya damu na upandikizaji wa figo.
Baadhi ya wataalamu wakiwa kwenye mkutano huo.
Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Damu, Dkt. Stella Rwezaura akiwasilisha mada kuhusu uanzishaji wa kituo cha kupandikiza uloto.
Afisa Mtekinolojia wa Maabara Kuu ya Muhimbili, Bw. Musa Suko akitoa taarifa kuhusu mashine mbalimbali ambazo zitatumika wakati wa kupandikiza uloto kwa wagonjwa wenye matatizo ya saratani.
Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Makubi na Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Prof. Museru wakitoka wodini kuwajulia hali wagonjwa.
Serikali imepongeza jitihada zinazofanywa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kuhusu uanzishwaji wa huduma za kibingwa ikiwamo huduma ya kupandikiza figo na uloto kwa wagonjwa wenye saratani ya damu.
Juhudi za upanuzi wa miundumbinu ya kutoa huduma za kibingwa, zimesaidia huduma za kibingwa kupatikana hapa nchini na kupunguza rufaa za wagonjwa kutibiwa nje ya nchi.
Pongezi hizo, zimetolewa na Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Abel Makubi wakati alipofanya ziara ili kuona na kupata taarifa kuhusu hatua ambayo Muhimbili imefikia kwenye maandalizi ya kupandikiza Uloto (Bone MarrowTtransplant) kwa wagonjwa wa Saratani ya damu na Selimundu.
“Kuna mageuzi makubwa sana yamefanyika kwenye kuboresha huduma za kawaida na kuanzisha huduma za kibingwa, miaka ya zamani kulikuwa na malalamiko, lakini hivi sasa hakuna tena kwa sababu tumepiga hatua,” amesema Prof. Makubi.
Prof. Makubi amesema ameona jinsi maandalizi ya kupandikiza Uloto yanavyokwenda vizuri na kwamba kilichobaki ni ununuzi wa mashine moja tu ili huduma hiyo iweze kuanza kutolewa kwa watu wenye uhitaji.
Mganga Mkuu ameutaka uongozi wa Hospitali kufanya jitihada ili ikiwezekana huduma ya kupandikiza uloto ianze mwezi Mei, mwaka huu.
Kuhusu changamoto ambazo zinaikabili Hospitali na sekta ya afya kwa ujumla, Prof. Makubi amesema zinaendelea kufanyiwa kazi.
Prof. Makubi amefafanua kwamba changamoto zitaendelea kutatuliwa ili kuhakikisha vipaumbele na sera za afya zinatekelezwa kwa lengo la kutoa huduma bora za afya kwa wananchi.
Katika hatu nyingine, Prof. Makubi ametoa wito kwa wataalamu wa afya nchini kujikita zaidi katika eneo la utafiti na ugunduzi ili kuja na majibu kuhusu namna ya kupambana na maradhi mbalimbali hasa katika kipindi hiki ambacho Dunia inapambana kutafuta chanjo na tiba ya maradhi mbalimbali.
Awali, akimkaribisha Mganga Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Lawrence Museru alisema kuanzia mwaka 2016 hospitali ilijikita kwenye kuboresha huduma na kuanzisha tiba za kibingwa ikiwemo upandikizaji figo, upandikizaji wa vifaa vya kusaidia kusikia na tiba radiolojia ambazo zilipunguza rufaa za wagonjwa kutibiwa nje ya nchi hivyo kuipunguzia Serikali gharama kubwa za matibabu.
Toa Maoni Yako:
0 comments: