Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akisalimiana na Meneja Mipango Mwandamizi wa Shirika la Save The Children Tanzania (SCT) Florian Fanuel na  Afisa Mradi Mkuu wa WFP, Florian Ngali katika Maonesho ya  Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani yanayofanyika Kitaifa mkoani Singida. 
 Mkuu wa Mkoa wa Singida,  Dkt.Rehema Nchimbi akipima uzito katika banda la Mashirika ya  Save the Children Tanzania, Shirika la chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) katika Maonesho ya  Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani yanayofanyika Kitaifa mkoani Singida leo. Kutoka kushoto ni  Msaidizi wa Ofisi ya FAO, Mihambo Gabriel na Afisa Mradi Mkuu wa WFP, Florian Ngali.
 Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Rehema Nchimbi akipima uzito.
 Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Rehema Nchimbi akizungumza na waandishi wa habari.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Kilimo, Revocatus Kassimba, akizungumzia kukamilika kwa maandalizi ya maadhimisho hayo.
 Mwalimu Elias Bubimbi kutoka Chuo cha Kilimo Mati- Mubondo (kulia) akimuelekeza  mwananchi aliyetembelea banda la chuo hicho jinsi ya kutengeneza biskuti za mbaazi.
 Afisa Mifugo Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Deograsias Ruzangi akitoa maelezo kwa  Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Rehema Nchimbi alipotembelea banda la wizara hiyo.
 Majasiriamali Rosemary Luhasile kutoka Nantakunganirwa Group akimpa zawadi ya dagaa Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Rehema Nchimbi.

 Afisa Mfawidhi Kituo cha Wizara cha Ukuzaji Viumbe Maji (Mwamapuli) akimuelekeza jinsi ya ufugaji wa samaki Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Rehema Nchimbi alipotembelea banda la kituo hicho. Wa tatu kutoka kulia ni Mzee Juma  Ibrahim Mkhofoi mfugaji maarufu wa samaki mkoani Singida.
Afisa Ubora Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB), Idd Mkolamasa, akimuelekeza jambo Mkuu wa Wilaya ya Singida, Paskas Muragili alipotembelea banda la CPB.

Dotto Mwaibale na Boniphace Jilili, Singida 

SHIRIKA la Save the Children Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limeendesha zoezi la upimaji wa uzito na urefu kwa wananchi katika maonesho ya maadhimisho ya siku ya chakula duniani ambayo kitaifa yanafanyika mkoani Singida. 


Akizungumza na waandishi wa habari leo Meneja Mipango Mwandamizi wa shirika hilo, Florian Fanuel alisema wanafanya zoezi hilo katika maonesho hayo kupitia mradi wa boresha lishe ambao unaiwezesha jamii kujenga lishe bora na kuondokana na utapiamlo na lishe duni. 

"Hapa tunaonesha jinsi ambavyo jamii inaweza kujizalishia chakula chenye lishe bora lakini pia tunatumia fursa ya maadhimisho haya kutoa elimu na huduma za lishe"alisema Fanuel. 

Wakati huo huo  mkuu wa mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi  akizungumza baada ya kupima  uzito na urefu aliwahimiza wananchi wa mkoa huo na wa mikoa ya jirani kufika kwenye maonesho  hayo ili kupata elimu hiyo.

Alisema kupitia maonesho hayo ni vyema kila mwananchi kujitathimini juu ya lishe aliyonayo kuwa yuko sawa kilishe ama laa  baada ya kupata elimu kutoka kwa wataalamu hao. 

"Watanzania wengi hawathamini afya zao, mtu yuko tayari kumiliki gari zuri, nguo nzuri lakini anasahau lishe " alisema Dkt Nchimbi. 

Nchimbi alisema pamoja na kupata elimu ya lishe pia maonesho hayo yanatoa fursa ya wananchi kupata elimu ya utunzaji wa ardhi,matumizi ya mbegu sahihi ili kuongeza kiwango cha uzalishaji.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Kilimo,  Revocatus Kassimba alisema maandalizi ya maonesho hayo yamekamili na lengo hasa ni kuwapa elimu ya lishe wananchi ili kuondokana na lishe duni.

Alisema takwimu zinaonyesha uzalishaji wa chakula unatosheleza, hivyo watanzania hawana haja ya kuwa na lishe duni, ni elimu tu ambayo inahitajika ya namna ya kutumia vyakula wanavyovizalisha ili wawe na lishe bora. 
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: