Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Mkewe Mama Janeth Magufuli watatu kutoka kulia Balozi wa Japan hapa nchini Shinichi Goto watatu kutoka kushoto aliyeshika utepe, Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB nchini Tanzania Dkt. Alex Mubiru wasita kutoka kulia aliyeshika utepe pamoja na Viongozi wa Mkoa wa Mtwara, Wabunge, akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Barabara ya Mangaka- Nakapanya-Tunduru km 137 pamoja na Barabara ya Mangaka- Mtambaswala km 65.5 sherehe zilizofanyikka katika Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwapongeza wadau wa Maendeleo, Balozi wa Japan hapa nchini Shinichi Goto pamoja na Mwakilishi Mkazi wa benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB nchini Tanzania Dkt. Alex Mubiru mara baada ya kufungua barabara ya Mangaka-Nakapanya-Tunduru km 137 pamoja na Barabara ya Mangaka-Mtambaswala km 65.5 katika Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwapungia mkono wananchi wa Nanyumbu mara baada ya kufungua barabara ya Mangaka-Nakapanya- Tunduru km 137 pamoja na Barabara ya Mangaka-Mtambaswala km 65.5 katika Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara.




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mikangaula iliyopo Nanyumbu mkoani Mtwara wakati akielekea Mangaka kwenda kufungua barabara.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwasalimia wananchi wa Nanyumbu mara baada ya kuwasili kutoka Masasi kwa ajili ya kufungua barabara ya Tunduru-Mangaka-Mtambaswala yenye jumla ya km202.5.

PICHA NA IKULU.

Na Mwandishi Wetu - MAELEZO.

RAIS Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Watanzania kuacha kulalamika na badala yake imewataka wananchi wa mikoa ya kusini kutambua kuwa Serikali itaendelea kuwatumia na kuwaletea maendeleo katika sekta za kijamii na kiuchumi ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa barabara ya Tunduru-Nakapanya-Mangaka- Mtambaswala yenye urefu wa kilometa 202.5, Rais Magufuli alisema Serikali yake itaendelea kuwajibika na kusimamia miradi ya maendeleo inayobeba manufaa kwa Watanzania walio wengi.

Alisema kuwa Wananchi wa mikoa ya Kusini wanapaswa kutambua historia ya ujenzi wa barabara hiyo ulianzia katika Serikali za Awamu zilizopita ambapo kulikabiliwa na changamoto mbalimbali wakati wa kuomba fedha kutoka wafadhili na wadau wa maendeleo.

Aidha Rais Magufuli aliwataka wananchi wa Mkoa wa Mtwara kuendelea kuiunga mkono Serikali katika juhudi mbalimbali inazofanya za kuimarisha miundombinu ya barabara katika ukanda wa kusini ikiwemo Mtwara kwani hapo awali hali ya miundombinu hiyo haikuwa ya kuridhisha ukilinganisha na ilivyo sasa.

‘Mtakumbuka kuwa wakati tulipokuwa tukiomba fedha za ujenzi wa daraja la Umoja lilnalounganisha Tanzania na Msumbiji ambalo ndio kiungo muhimu baina ya mataifa haya, wafadhili wote walikataa kutoa fedha kwani daraja hili linaingia porini katika kila nchi, lakini tulisimama imara na kujenga daraja hili’ alisema Rais Magufuli.

Alisema kutokana na Mkoa wa Mtwara kuwa katika ukanda muhimu katika usafirishaji wa bidhaa muhimu za kiuchumi kupitia bandari, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Japan (JICA) na Benki ya Mandeleo ya Afrika (AfDB) zilikubaliana kujenga barabara hiyo ambayo kwa sasa itakuwa imefungua fursa za ukanda wa kiuchumi kwa kushirikiana na nchi ya Msumbiji.

‘Ukitazama fedha hizi, si ndogo kwa mfano kipande cha Tunduru-Nakapanya-Mangaka yenye urefu wa kilometa 137 kimetumia wakandarasi watatu na washauri 3 na jumla ya Tsh Bilioni 182 zimetumika, na kipande cha Mangaka- Mtambaswala chenye urefu wa kilometa 56 pia kiasi cha Tsh Biloioni 56 kimetumika’ alisema Rais Magufuli.

Alisema kuwa kitendo cha wadau hao wa maendeleo kuiunga mkono Tanzania kinatokana na imani waliyonayo kwa Serikali ya Awamu ya Tano, kwani yapo mataifa mbalimbali ya Bara la Afrika yanayohitaji kujengewa barabara na kupatiwa misaada mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.

Kuhusu Kipande cha barabara ya Masasi-Mtwara chenye urefu wa kilometa 150, Rais Magufuli amewaagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Waziri wa Fedha na Mipango kuandika barua ya mchanganuo wa maombi ya fedha kwa Shirika la Maendeleo ya Japan (JICA) NA Benki ya Maendeleo ya Afrika ili kuanza mara moja ujenzi wa barabara hiyo.

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe alisema kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo kumeweza kutimiza malengo ya Serikali ya kuiunganisha ushoroba wa kusini katika kiwango cha lami.

Aliongeza kuwa katika ujenzi huo, Shirika la Maendeleo ya Japan ilichangia asilimia 32.83, Benki ya Maendeleo ya Afrika 64.79 na Serikali ya Tanzania ilitoa asilimia 2.38 ikiwemo malipo ya fidia kwa wananchi pamoja na kodi.

Naye Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Alex Mubiru alisema kufunguliwa kwa barabara hiyo kumeweza kutimiza ndoto ya waasisi wa Mataifa ya Tanzania na Msumbiji Samora Machel na Julius Nyerere, ambapo walitaka mataifa hayo kuweza kuunganisha na Daraja la Umoja ambalo kwa sasa litatoa fursa kwa wananchi wote kuweza kuimarisha shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: