ACCRA, GHANA | Februari 28, 2026

Rais Mstaafu wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, ameshiriki katika hafla ya utoaji wa Tuzo za Viongozi Bora barani Afrika 2026 zilizofanyika jijini Accra, akimkabidhi tuzo Waziri Mkuu wa Lesotho, Samuel Matekane, pamoja na viongozi wengine waliotambuliwa kwa mchango wao katika maendeleo ya bara hilo.

Tuzo hizo huandaliwa na Africa Leadership Magazine kwa kushirikiana na Africa Leadership Organisation, taasisi ambayo Dkt. Kikwete ni Mwenyekiti wa Bodi yake ya Ushauri.
Mshindi wa jumla wa mwaka huu alikuwa Rais wa Ghana, John Dramani Mahama, aliyepokea Tuzo ya Mwafrika wa Mwaka 2026 kutokana na mchango wake katika kukuza demokrasia, uchumi na ushirikiano wa kikanda, hususan kupitia utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).

Akizungumza kabla ya kukabidhi tuzo ya mshindi mkuu, Dkt. Kikwete alisema uongozi bora hupimwa kwa uwezo wa kuboresha maisha ya wananchi.

“Kila kizazi cha uongozi hukutana na changamoto zake, na mafanikio hupimwa kwa uwezo wa kuinua kipato cha watu na hali zao za maisha,” alisisitiza.

Tuzo ya Rais Mahama ilipokelewa kwa niaba yake na Mwanasheria Mkuu wa Ghana, Dominic Akuritinga Ayine, huku Mkuu wa Majeshi wa Uganda, Muhoozi Kainerugaba, akipata tuzo ya uongozi wa kijeshi iliyopokelewa na msemaji wa jeshi hilo.

Viongozi wengine waliotunukiwa ni pamoja na Rais wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah, aliyeshinda tuzo ya kiongozi bora wa kisiasa, na Makamu wa Rais wa Angola, Esperança da Costa, aliyepokea tuzo ya kiongozi bora mwanamke barani Afrika.

Kwa mujibu wa waandaaji, jumla ya tuzo 36 zilitolewa mwaka huu, zikihusisha viongozi wa siasa, diplomasia, biashara, ulinzi na tasnia nyingine, baada ya mchakato wa mapendekezo na kura za mtandaoni.

Hafla hiyo imeendelea kuimarisha hadhi yake kama jukwaa la kutambua viongozi wanaochangia maendeleo ya Afrika na kuhamasisha kizazi kipya cha viongozi wenye maono ya kuendeleza bara hilo.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: