Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ameongoza kikao maalum cha kutafuta suluhu ya mgogoro kati ya wachimbaji wadogo na uongozi wa Mgodi wa Ililika uliopo Nyarugusu, mkoani Geita, akisisitiza umuhimu wa haki na uwazi katika sekta ya madini.

Kikao hicho kilifanyika Februari 20, 2026 jijini Dodoma, kikihusisha wawakilishi wa wachimbaji wadogo wa duara namba 15 pamoja na uongozi wa mgodi huo.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Waziri Mavunde alieleza kuwa ili kufikia muafaka wa kudumu ni lazima uchunguzi wa kitaalamu ufanyike. Aliagiza kupimwa kwa sampuli za mawe yanayolalamikiwa ili kubaini ukweli wa madai yaliyotolewa na wachimbaji, huku pia akisisitiza uwepo wa mashahidi zaidi kutoka pande zote ili kusaidia upatikanaji wa taarifa sahihi.

“Lengo letu ni kuhakikisha haki inapatikana kwa kila upande na kwamba shughuli za uchimbaji zinaendelea kwa utaratibu unaozingatia sheria na maslahi ya taifa,” alisema Waziri Mavunde wakati wa kikao hicho.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhan Lwamo, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita Samweli Shoo, Msimamizi wa Mgodi wa Ililika Bi. Salma Mipawa pamoja na mwakilishi wa wachimbaji wadogo Bw. Geofrey Mushi.

Mgogoro huo umeelezwa kuwa uliibuka kufuatia malalamiko ya wachimbaji kuhusu umiliki na thamani ya mawe yaliyopatikana katika eneo hilo, jambo lililosababisha kusitishwa kwa baadhi ya shughuli za uchimbaji.

Hatua ya Waziri kuingilia kati imepokelewa vyema na wadau wa sekta ya madini, wakiamini kuwa itasaidia kurejesha utulivu na kuimarisha ushirikiano kati ya wachimbaji wadogo na wawekezaji wakubwa.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: