Na Mwandishi Wetu.
Matumaini ya timu ya taifa ya Nigeria, Super Eagles, kufuzu Kombe la Dunia 2026 yamepata msukumo mpya kufuatia shinikizo linaloendelea ndani ya uongozi wa Shirikisho la Soka Afrika, CAF.
Hali hiyo inakuja wakati Nigeria ikiendelea kusubiri uamuzi wa Shirikisho la Soka Duniani, FIFA, kuhusu malalamiko yao dhidi ya timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DR Congo, kwa madai ya kutumia wachezaji wasioruhusiwa katika mechi ya mchujo wa Afrika.
Shirikisho la Soka la Nigeria (NFF) liliwasilisha malalamiko hayo Desemba mwaka jana likidai kuwa DR Congo huenda ilitumia hadi wachezaji sita wenye dosari katika vibali vyao wakati wa fainali ya mchujo iliyochezwa nchini Morocco. Katika mchezo huo, Nigeria ilipoteza kwa penalti 4-3, matokeo yaliyozima ndoto zao za kufuzu moja kwa moja hatua ya mchujo wa mabara.
Hata hivyo, hali mpya imejitokeza baada ya Rais wa Chama cha Soka cha Mauritius, Samir Sobha, kumtaka kuondolewa kwa Katibu Mkuu wa CAF, Véron Mosengo-Omba, akidai hana mamlaka ya kisheria kuendelea kushika wadhifa huo. Mosengo-Omba anatoka DR Congo, jambo ambalo baadhi ya wadau wanaamini linaweza kuibua mgongano wa maslahi katika kushughulikia malalamiko ya Nigeria.
Sobha amenukuliwa akisisitiza kuwa CAF inapaswa kuheshimu katiba na taratibu zake za kiutawala ili kuhakikisha maamuzi yote yanafanyika kwa uwazi na uhalali.
Wakati huo huo, NFF pamoja na Tume ya Michezo ya Nigeria wameeleza kuwa bado hawajapokea taarifa rasmi kutoka FIFA kuhusu hatima ya malalamiko yao, wakitoa wito kwa umma kupuuza taarifa zisizo rasmi zinazosambazwa mtandaoni.
Iwapo FIFA itaamua kuipatia Nigeria ushindi wa mezani au kuadhibu DR Congo, hatua hiyo inaweza kufungua mlango kwa Super Eagles kushiriki mechi za mchujo wa mabara kuelekea Kombe la Dunia 2026, jambo litakalofufua matumaini ya taifa hilo kurejea katika mashindano makubwa zaidi ya soka duniani.
Sakata hilo linaendelea kufuatiliwa kwa karibu barani Afrika huku wadau wakisubiri uamuzi wa mwisho wa FIFA ambao unaweza kubadilisha ramani ya uwakilishi wa Afrika katika fainali za Kombe la Dunia.



Toa Maoni Yako:
0 comments: