Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Tanga (TangaUWASA), Mhandisi Geofrey Hilly,akitoa maelezo ya Mradi wa maji wa Hatifungani ya Kijani kwa Madiwani waa Halmashauri ya Jiji la Tanga walipofanya ziara ya kikazi katika kituo cha kuzalisha maji Mowe Februari 5, 2026.
Na Dotto Mwaibale, Tanga
MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (TangaUWASA) imeendelea na zoezi maalum la kufunga mita za malipo kabla (Pre-paid Meters) katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Tanga, hatua inayolenga kuboresha ukusanyaji wa mapato na kudhibiti matumizi ya maji.
Taarifa hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa TangaUWASA, Mhandisi Geofrey Hilly, alipokuwa akizungumza na Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Tanga katika kikao cha wadau kilichofanyika Februari 5, 2026 kwa lengo la kuwajengea uwezo na kuwasilisha taarifa ya maendeleo ya upatikanaji Huduma.
Kabla ya kikao hicho, Waheshimiwa Madiwani walipata fursa ya kutembelea na kujionea maendeleo ya utekelezaji Mradi wa Hatifungani wenye thamani ya Shillingi Bilioni 53.12 unaotekelezwa katika kituo cha Kuzalisha maji Mowe na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2026.
Mhandisi Hilly alisema mradi huo umelenga kuimarisha upatikanaji wa huduma ya uhakika kwa wananchi kwa saa 24 na aliongeza kuwa hadi sasa zaidi ya mita za malipo kabla 4,500 tayari zimesambazwa na kufungwa kwa wateja na kuwa mita hizo zinamsaidia mteja kutumia kiasi cha maji kulingana na fedha aliyolipia, hivyo kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.
Aliongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo una lenga kuongeza uwezo wa uzalishaji na usambazaji wa maji kutoka mita za ujazo 45,000 kwa siku zilizopo sasa hadi kufikia mita za ujazo 60,000 kutokana na uboreshaji wa miundombinu ya Mtambo, ulazaji wa mabomba makubwa yenye kipenyo cha milimita 600, upanuzi wa kituo cha kusafisha na kutibu maji cha Mowe, ujenzi wa tangi kubwa la kuhifadhi maji lenye mita za ujazo 35,000 pamoja na kuimarisha utunzaji na uhifadhi wa vyanzo vya maji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TangaUWASA, Dk. Fungo Ali Fungo, alisema kikao hicho ni mwanzo mzuri wa ushirikiano wa karibu kati ya mamlaka na Madiwani, akisisitiza kuwa mikutano hiyo itakuwa ni utaratibu wa kawaida.
“Tutakutana mara kwa mara kwa kuwa Madiwani ni kiungo muhimu kati yetu na wananchi. Maswali mengi ya wananchi huanzia kwao, hivyo ni muhimu kuwa na majadiliano ya karibu,” alisema Dk. Fungo.
Aliongeza kuwa kikao hicho kililenga pia kuwajengea Madiwani uelewa wa kazi zinazotekelezwa na TangaUWASA ili kuwa na uelewa wa pamoja na ufahamu mzuri wa yote yanayoendelea katika kufanikisha adhma ya Serikali ya upatikanaji wa huduma ya uhakika kwa wananchi.
Nae kwa upande wake Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga, Mhe. Selebosi Mustafa, aliipongeza TangaUWASA kwa kuandaa kikao kazi hicho mapema baada ya madiwani kuapishwa, akisema ni mfano mzuri wa taasisi kujenga uelewa na kuimarisha ushirikiano na viongozi wa wananchi.
Alisema lengo ni kujenga uhusiano, kuimarisha uwakilishi wa mamlaka kwa wananchi na kuwapa madiwani nafasi ya kushiriki kikamilifu katika kusimamia huduma za maji. Aidha, alishauri TangaUWASA kupanga muda wa kutosha kwa ajili ya madiwani kutembelea miradi yote ya maji na vyanzo vyake ili kujionea hali halisi ya kazi zinazotekelezwa.
Katika kikao hicho, madiwani walipata fursa ya kuuliza maswali na kutoa maoni mbalimbali yaliyojibiwa na Mhandisi Geofrey Hilly kwa kushirikiana na wataalamu wa Mamlaka hiyo.
Katika hatua nyingine, Madiwani walimpongeza Afisa Uhusiano wa TangaUWASA, Bi. Devotha Mayala, kwa utendaji kazi wake uliotukuka, wakisema amekuwa akipokea simu na kutoa msaada kwa wakati wowote.
“Kwa kweli nichukue nafasi hii kumpongeza Devotha kwa kazi kubwa anayoifanya mchana na usiku kwa kuwasikiliza wateja na kutatua changamoto zinazowasilishwa.
Naibu Mstahiki Meya na Diwani wa Kata ya Mwanzange, Khalid Hamza akifunga kikao hicho.


Toa Maoni Yako:
0 comments: