
Kupitia ujumbe wake aliouandika kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram, Dkt. Gwajima amesema jamii imezoea maisha ya kulumbana mitandaoni na kusherehekea hadhi bila utaratibu, hali ambayo imechangia kuporomoka kwa maadili, hasa miongoni mwa vijana wa kike.
Akiuliza maswali ya kujitathmini, waziri huyo alisema ni muhimu kujihoji ni nani anayepaswa kuwajibika zaidi katika kukuza maadili kwa watoto, akitaja wazazi, jamii na mifumo ya malezi kuwa na jukumu kubwa.
“Tujiulize, je, tuanze kufunga kliniki za maadili au makanisani na misikitini pawepo mahudhurio ya lazima? Au wengine wanafikiri hadi Polisi ndipo pa kushughulikia masuala ya maadili?” alihoji.
Dkt. Gwajima alisisitiza kuwa suluhisho la kudumu si adhabu wala lawama, bali ni uwezeshaji wa wanawake kiuchumi na kijamii, akisema serikali tayari imetenga zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa ajili ya mikopo na programu za uwezeshaji wanawake nchini.
Alitoa wito kwa wadau wote kuacha mijadala isiyo na tija na badala yake kuelekeza nguvu kwenye kuanzisha na kuimarisha programu za ujasiriamali na maendeleo ya wanawake kuanzia ngazi ya kijiji, mtaa, kata, halmashauri hadi mkoa.
“Kama tunapenda maneno, tuyageuze vitendo. Twendeni tukajenge mazingira ya mwanamke chanya wa maendeleo, mwenye maadili na mchango chanya kwa taifa,” alisisitiza.
Waziri huyo pia aliwataka Watanzania kuacha kushabikia mijadala ya mitandaoni isiyo na suluhisho, akibainisha kuwa kujenga taifa lenye wanawake wenye maadili kunahitaji mshikamano wa jamii nzima.
Dkt. Gwajima alihitimisha kwa kusisitiza kuwa yeye ni mlezi wa kizazi kijacho na ana dhamira ya dhati ya kuona Tanzania inajenga wanawake wenye misingi imara ya maadili, uzalendo na maendeleo endelevu.


Toa Maoni Yako:
0 comments: