
Akizungumza kuhusu mpango huo, Mkuu wa Kitengo cha Uendelezaji Michezo wa BMT, Bw. Benson Chacha, alisema ziara hiyo inalenga pia kuhakikisha kuwa Kamati za Michezo za Mikoa zinatimiza wajibu wao wa kusimamia na kuendeleza sekta ya michezo katika ngazi za mikoa.
Kwa mujibu wa Bw. Chacha, Kamati za Michezo za Mikoa hujumuisha Afisa Tawala wa Mkoa husika, Afisa Michezo wa Mkoa, Wajumbe saba walioteuliwa na Mkuu wa Mkoa, pamoja na mjumbe mmoja kutoka kila chama au shirikisho la michezo lililosajiliwa katika mkoa husika. Aidha, Maafisa Tawala wa Wilaya na Maafisa Michezo wa wilaya zote za mkoa husika ni wajumbe wa kamati hizo.
Alisema kamati hizo ndizo zenye jukumu la kutekeleza majukumu ya Baraza la Michezo la Taifa katika ngazi ya mikoa, ikiwamo usajili wa vyama na vilabu, usimamizi wa shughuli za michezo, uendelezaji wa vipaji, uimarishaji wa miundombinu ya michezo, pamoja na kuratibu mashindano mbalimbali.
Bw. Chacha alitaja mikoa itakayotembelewa kuwa ni Kagera, Shinyanga, Simiyu, Mara, Mwanza, Geita, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Singida na Tabora.
Aliongeza kuwa tathimini hiyo inalenga pia kupima utayari wa kamati hizo katika kuendeleza sekta ya michezo, ili kuchangia kuongeza ajira, kuimarisha amani na mshikamano wa jamii, kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika michezo, na kufikia matarajio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Tunataka kuona ni kwa namna gani Kamati za Michezo za Mikoa zimejipanga kuendesha michezo kwa kuzingatia misingi ya kitaifa, sambamba na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia michezo,” alisema Bw. Chacha.
Aidha, alisema tathimini hiyo itaangalia hatua zilizochukuliwa na kamati hizo katika kuimarisha utawala bora, uwazi na uwajibikaji, hususan katika kusimamia shughuli za vyama na mashirikisho ya michezo ili viendeshwe kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo.
Bw. Chacha alisisitiza kuwa BMT itaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wa michezo katika ngazi zote ili kuhakikisha sekta ya michezo nchini inaendelea kukua kwa tija na kuchangia maendeleo ya Taifa kwa ujumla.


Toa Maoni Yako:
0 comments: