Buyu, Zanzibar

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali imedhamiria kufanya mageuzi makubwa katika sekta za elimu, sayansi, utafiti na ubunifu ili kujenga uchumi imara, shindani na endelevu, unaowanufaisha Watanzania kwa upana zaidi.

Rais Samia ameyasema hayo Januari 8, 2026, katika eneo la Buyu, visiwani Zanzibar, mara baada ya kuzindua Jengo la Taaluma na Utawala la Taasisi ya Sayansi za Bahari Zanzibar (UDSM–IMS). Amesisitiza kuwa taasisi hiyo ni mdau muhimu wa Serikali katika kukuza uchumi shirikishi, hususan uchumi wa buluu, unaotegemea rasilimali za bahari.

Amesema uwepo wa IMS utaimarisha uvuvi endelevu, utalii wa baharini, pamoja na ulinzi na matumizi bora ya rasilimali za bahari, hivyo kuchangia moja kwa moja katika kukuza pato la Taifa na ustawi wa wananchi.
Katika hotuba yake, Rais Samia ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa usimamizi mzuri wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), akisema mradi huo umeleta matokeo chanya katika miundombinu na ubora wa elimu ya juu nchini. Aidha, amewahimiza vijana kutumia fursa zilizopo kupata elimu na ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira.

Rais pia amewapongeza viongozi na watumishi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa kukamilisha mradi huo kwa wakati na kwa viwango vya juu, huku akiishukuru Benki ya Dunia kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa Mradi wa HEET.

Aidha, amewataka wahadhiri na watafiti kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi ili tafiti na bunifu zitakazofanywa ziweze kuleta matokeo ya moja kwa moja katika maendeleo ya Taifa. Vilevile, amewahimiza wanafunzi kuwa walinzi na mabalozi wa rasilimali za bahari kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amesema ameiomba Serikali kushirikiana na Benki ya Dunia ili kuanzisha Awamu ya Pili ya Mradi wa HEET, itakayowezesha kukamilisha maeneo ya utekelezaji ambayo bado hayajakamilika.

Dkt. Kikwete amesema majengo mapya yaliyozinduliwa ni msingi muhimu wa kuendeleza tafiti za kisasa, kutoa mafunzo bora na kukuza uchumi wa buluu, sambamba na kuchochea maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye, amesema uwekezaji huo utaongeza kwa kiasi kikubwa idadi ya wanafunzi katika Taasisi ya Sayansi za Bahari (IMS). Amesema kwa sasa IMS ina uwezo wa kudahili takribani wanafunzi 172 kwa mwaka, lakini baada ya kukamilika kwa miundombinu hiyo, uwezo utaongezeka hadi wanafunzi 472 kwa mwaka, sawa na ongezeko la wanafunzi 300.

Prof. Anangisye ameongeza kuwa IMS inaingia awamu mpya ya maendeleo kufuatia uzinduzi wa miundombinu ya kisasa katika eneo la Buyu, pamoja na kuimarishwa kwa vituo vya Mizingani na Pangani, hatua itakayoongeza uwezo wa taasisi katika kufundisha, kufanya tafiti na kuendeleza bunifu zitakazochangia maendeleo ya Taifa.
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: