Na WMJJWM – Dodoma

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, ametambuliwa rasmi kuwa miongoni mwa Wanawake 100 Wanaoheshimiwa wa Asili ya Afrika kwa mwaka 2026, kutokana na mchango wake mkubwa katika uongozi na maendeleo ya kijamii nchini na barani Afrika kwa ujumla.

Tuzo hiyo hutolewa na Kongamano la Wanawake wa Afrika (Africa Women Summit) kama heshima maalum kwa wanawake waliodhihirisha uongozi wa kipekee, uadilifu wa hali ya juu na mchango chanya katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa. Orodha hiyo inalenga kuenzi wanawake wanaovunja vikwazo, kubadilisha simulizi za maendeleo na kuhamasisha kizazi kijacho cha viongozi wanawake.

Katika toleo la mwaka 2026, wanawake mashuhuri kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika wametambuliwa, huku Tanzania ikiwakilishwa na Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, kutokana na juhudi zake katika kuendeleza usawa wa kijinsia, uwezeshaji wa wanawake, ulinzi wa watoto na ujumuishaji wa makundi maalum katika mipango ya maendeleo ya taifa.

Akizungumza baada ya kutambuliwa, Dkt. Gwajima amesema heshima hiyo ameipokea kwa shukrani kubwa, akimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa kinara wa uwezeshaji wa wanawake duniani na kwa kuendelea kuwaamini na kuwapa nafasi wanawake kushika nafasi za uongozi. Amesema utambuzi huo ni matokeo ya imani na malezi ya kiuongozi aliyopata chini ya Rais Samia.

Dkt. Gwajima ameahidi kuendelea kuchochea utekelezaji wa falsafa ya Kazi na Utu kwa kujituma na kuhakikisha huduma na programu za wizara yake zinawafikia wananchi wote, hususan wanawake, watoto na makundi yenye mahitaji maalum, ili kuenzi heshima hiyo na kutimiza maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa muda wake katika uongozi, Dkt. Gwajima amekuwa mstari wa mbele katika kuongoza mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, kuimarisha ulinzi wa mtoto, kukuza usawa wa kijinsia na kuhakikisha makundi maalum yanajumuishwa kikamilifu katika mipango na fursa za maendeleo, hatua zilizomjengea heshima kubwa ndani na nje ya nchi.

Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: