Na Said Mwishehe, Michuzi TV, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata jumla ya kilogramu 9,689.833 za dawa za kulevya, pikipiki 11 na magari matatu likiwemo basi aina ya Scania la kampuni ya King Masai Tours lenye namba za usajili za Msumbiji AAM 297 CA, baada ya kubainika kuwa limekarabatiwa maalum kwa ajili ya kuficha dawa hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 8, 2026 jijini Dar es Salaam, Kamishina Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema kuwa katika mtaa wa Wailes wilayani Temeke, mamlaka hiyo ilikamata pakiti 20 za dawa za kulevya aina ya skanka zenye uzito wa kilogramu 20.03.
Amesema dawa hizo zilikuwa zimefichwa ndani ya balo la mitumba na kusafirishwa kwa siri ndani ya basi hilo la Scania ambalo hufanya safari kati ya Nampula nchini Msumbiji na Tanzania.
“Uchunguzi umebaini kuwa nusu ya basi hilo ilikuwa imekarabatiwa mahsusi kwa ajili ya kuficha dawa za kulevya. Watuhumiwa waliokamatwa kuhusiana na tukio hili ni Amasha Iddi Mrisho (40), mkazi wa Buza jijini Dar es Salaam na Seleman Juma Ally (32), raia wa Msumbiji,” amesema Kamishina Jenerali Lyimo.
Ameongeza kuwa mmiliki wa basi hilo ni Mtanzania anayetambulika kwa jina la Martin Simon Kiando, ambaye kwa sasa anaendelea kuhojiwa na vyombo vya dola, akieleza kuwa kwa namna ambavyo basi hilo lilivyofanyiwa marekebisho makubwa, ni vigumu mmiliki kutojihusisha au kutojua kilichokuwa kinafanyika.
Kamishina Jenerali Lyimo ametoa onyo kali kwa wamiliki wa mabasi na vyombo vingine vya moto vinavyofanyiwa marekebisho kwa lengo la kusafirisha dawa za kulevya, akisisitiza kuwa mamlaka hiyo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama inaendelea kufuatilia kwa karibu na kwamba sheria itachukua mkondo wake bila muhali.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Halima Lutavi, amesema kuwa kufuatia tukio hilo, LATRA inamshikilia mmiliki wa basi hilo kwa hatua zaidi, huku akibainisha kuwa basi hilo halikuwa limesajiliwa kufanya kazi nchini Tanzania.
Amesema mmiliki wa basi aliwahi kuomba kulisajili nchini, lakini alishindwa kukidhi vigezo vilivyowekwa, hali iliyomlazimu kulisajili nchini Msumbiji.
“Basi hilo halikusajiliwa nchini kwa sababu baada ya kuomba usajili, mmiliki alitakiwa kuleta basi likaguliwe ili kuthibitisha kama linakidhi vigezo vya usalama na kiufundi. Pia ilitakiwa dereva awepo ili kuhakiki sifa zake na kuingizwa kwenye mfumo kwa kupewa kitufe cha dereva. Baada ya kupewa maelekezo hayo, hajarudi tena,” amesema Lutavi.
Ameeleza kuwa LATRA ina utaratibu wa kukagua mabasi yote kwa kuzingatia kadi ya ukaguzi inayoonesha muundo wa bodi ya gari, huku akisisitiza kuwa tukio hilo ni funzo na alama kwa mamlaka hiyo.
“Hata nchi nyingine zina vigezo vyao vya usajili wa mabasi. Tukio hili ni alamu kwetu, na kwa kushirikiana na mamlaka nyingine, tutafanya ukaguzi maalum ili kudhibiti mianya yote inayoweza kutumika kusafirisha dawa za kulevya,” amesema.



Toa Maoni Yako:
0 comments: