Mwenyekiti wa Mtandao wa Mabloga Tanzania (TBN), Beda Msimbe.

Na Mwandishi Wetu.

DAR ES SALAAM – Mtandao wa Mabloga Tanzania (TBN) umetoa shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuonyesha dhamira ya dhati ya kujenga taifa tulivu na lenye maendeleo, ambapo habari sahihi na zenye uwajibikaji zinatajwa kuwa nguzo kuu.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha mafunzo kwa mabloga kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe, alisema hatua ya Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuandaa mafunzo maalum kwa mabloga ni uthibitisho wa nia ya kuimarisha weledi wa uandishi wa habari za uchaguzi ili kulinda amani na utulivu wa taifa.

Msimbe alilaani vikali wale wanaokiuka maadili na utamaduni wa Kitanzania kwa kusambaza habari za uongo na uchochezi.

“Tupo tayari kuungana na Rais Samia kuhakikisha hakuna chokochoko zinazoweza kutishia uzalendo wetu,” alisema.

Alibainisha kuwa TBN, iliyoanzishwa mwaka 2015, itaendelea kutumia majukwaa yake kusambaza habari chanya na za maendeleo zinazounganisha juhudi za Serikali katika kujenga Tanzania mpya.

Mafunzo hayo yaliwashirikisha wataalamu mbalimbali waliotoa mada kuhusu Mwongozo wa Waandishi wa Habari katika Uandishi wa Habari za Uchaguzi (Dkt. Egbert Mkoko), Kanuni za Utangazaji wa Uchaguzi kwa Vyama vya Siasa (Mhandisi Andrew Kisaka), na Uhusiano kati ya Waandishi wa Habari na Jeshi la Polisi (DCP David Misime).

Vilevile, mada nyingine ziliwasilishwa na Bi. Rehema Mpagama kuhusu Maadili na Sheria kwa Waandishi wa Habari, Dkt. Darius Mukiza kuhusu Matumizi ya Mitandao ya Kijamii na Akili Mnemba (AI) kuelekea uchaguzi, na Bw. Innocent Mungy kuhusu Ulinzi wa Taarifa Binafsi.

Msimbe pia alisisitiza nafasi ya mabloga katika kujenga hifadhidata ya taarifa sahihi za Tanzania kwa ajili ya kufundisha AI, akieleza kuwa teknolojia hiyo inapaswa kutumika kama nyenzo ya kusaidia, na si mbadala wa ubunifu wa mwanadamu.

Alishukuru Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa mchango wake katika kufanikisha mafunzo hayo na kuwataka mabloga kuendelea kufanya kazi kwa uaminifu, weledi na uwajibikaji, “wakikumbuka kuwa kuna maisha kabla ya uchaguzi na baada ya uchaguzi.”
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: