

Na Mwandishi Wetu.
Dodoma. Machi 18, 2025. Kampuni ya Puma Energy Tanzania imezindua PumaGas jijini Dodoma, hatua inayoonyesha dhamira yake katika kuhakikisha suluhisho la nishati nafuu na ya uhakika kwa matumizi ya nyumbani na kibiashara nchini Tanzania. Hatua hii inadhihirisha uungaji mkono wa kampuni wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024 2034), uliozinduliwa Mei 2024 na Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Kimataifa kuhusu Nishati Safi ya Kupikia jijini Paris ulioandaliwa na Shirika la Nishati Duniani (IEA).
Waziri wa Madini na Mbunge wa Dodoma Mjini, Mhe. Anthony Mavunde, amehudhuria uzinduzi huo na kuipongeza kampuni hiyo kwa kuwa mdau mkubwa wa kuunga mkono jitihada za serikali za kukuza na kuwezesha upatikanaji wa huduma ya nishati safi nchi nzima na kuhakikisha ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.
“Napenda kuwapongeza wadau wetu wakubwa wa huduma na bidhaa za nishati nchini, Puma Energy Tanzania, kwa kuendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha wananchi maeneo mbalimbali wanafikiwa na huduma za uhakika. Ushirikiano kati ya sekta za umma na binafsi ni muhimu katika kufanikisha malengo ya kitaifa ya kukuza matumizi na kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi, hususani kwa maeneo ya vijijini ambayo bado upatikanaji wake unakumbana na changamoto mbalimbali,” amesema Mhe. Mavunde.

“Kiwango cha matumizi ya nishati safi nchini bado hakiridhishi kitu ambacho kinaathiri taifa kwa kiasi kikubwa hususani kimazingira na kiafya. Bado Watanzania wanategemea kuni na mkaa kupikia wakati rasilimali za nchi zinatosheleza kuwafanya waachane na mazoea haya. Uwekezaji huu wa Puma Energy Tanzania kupitia bidhaa yenu ya PumaGas utakuwa chachu ya kuwapatia wananchi chaguo rahisi na la uhakika la nishati kwa matumizi ya nyumbani na kibiashara. Ninawaomba pia uzinduaji wa huduma hii uendane na shughuli za utoaji elimu na uhamasishaji kwasababu bado watu wengi wanadhahania kuwa nishati safi ya kupikia ni gharama na sio salama. Kama serikali tuko nanyi bega kwa bega kuhakikisha mnalifanikisha hili na kuwafikia wananchi wengi zaidi hususani maeneo ya vijijini,” alimalizia Waziri wa Madini.
Uzinduzi wa nishati safi ya kupikia ya Puma Energy Tanzania ni sehemu ya kampuni hiyo ya kupanua wigo wa huduma hii ambayo kwa sasa inapatikana katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani pekee.

Akielezea kuhusu uzinduzi huu, Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Bi. Fatma Abdallah amebainisha kuwa wamejizatiti katika uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya uhifadhi, maeneo ya manunuzi, pamoja na mawakala wa usambazaji wa mitungi ya gesi.
"Uzinduzi huu unathibitisha dhamira yetu ya dhati katika kuunga mkono serikali kufikia lengo lake la mabadiliko ya suluhisho la nishati endelevu ambayo inaboresha afya ya umma na ustawi wa kiuchumi kwa kizazi cha sasa na kijacho. Mkakati wa Upikaji Safi wa Tanzania unalenga kufikia asilimia 80 ya watu kuhamia kwenye upikaji safi na kutoa wito kwa sekta binafsi kuongeza uwekezaji katika gesi safi asilia,” amesema Bi. Fatma Abdallah.
Aliongeza kuwa, “Gesi safi asilia ni njia salama, rahisi na ya gharama nafuu ya kuzipa jamii zetu nishati; kuwezesha upikaji safi na kupunguza madhara yanayotokana na matumizi ya nishati asilia za kupikia. Mbali na matumizi ya nyumbani, gesi safi ya kupikia pia ni chanzo muhimu cha nishati kwa matumizi ya kibiashara na viwandani, ikitumika katika hoteli, migahawa, hospitali, shule na maduka makubwa.”
“Watumiaji wa PumaGas wanahakikishiwa nishati mbadala ya uhakika, salama na bora, ambayo itapunguza utegemezi wa nishati asilia za kupikia kama vile mkaa na kuni, ambazo huchangia uharibifu wa mazingira. Hivyo, napenda kuualika umma na wadau wengine kuungana nasi katika mpango huu katika kupanua wigo wa upatikanaji wa suluhisho la nishati safi nchini kote,” alimalizia Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania.
Wateja wataweza kununua mitungi ya gesi katika vituo vyote vya huduma za kujaza mafuta Dodoma, pamoja na mawakala wa uuzaji wa rejareja. Kampuni pia inatarajia kuzindua maduka mawili ya kisasa ya PumaGas ambayo yatatoa huduma za kisasa, yakiwa na huduma mbalimbali ikiwemo kujaza na kubadilisha mitungi ya gesi, kuhakikisha watu hawakwami katika shughuli zao za kila siku.
Kama hiyo haitoshi, kwa kuanza rasmi upatikanaji wa huduma hii mpya jijini Dodoma, wateja watapatiwa ofa mbalimbali pindi wanunuapo mitungi ya gesi ya ujazo tofauti kama vile 6kg, 15kg, na 38kg. Kwa kuongezea, pia kampuni inategemea kuzindua huduma ya uuzaji wa uuzaji wa nishati kwa wingi au ujazo mkubwa kuanzia 200kg mpaka 20,000kg.
Toa Maoni Yako:
0 comments: