Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) Mhe. Augustine Vuma Holle (Mb) akizungumza mara baada ya Kamati hiyo kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato jijiji Dodoma leo Machi 12,2025.
Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta,akizungumza mara baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato jijiji Dodoma leo Machi 12,2025
Na Okuly Julius _ DODOMA
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato na kusema kuwa, uwanja huo ukikamilika utakuwa lango la uchumi kwa wananchi wa Dodoma na taifa kwa ujumla.
Akizungumza leo, Machi 12, 2025, katika ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Augustine Vuma Holle (Mb), amesema mradi huo ni wa kimkakati kwani fursa nyingi za kibiashara na kiuwekezaji zitaongezeka kupitia mradi huo.
"Katika mradi huu kuna miradi miwili ndani ya mradi mmoja, ambapo kuna ujenzi wa majengo kama jengo la abiria na jengo la kuongoza ndege lenye thamani ya zaidi ya bilioni 190, ambalo utekelezaji wake umefikia asilimia 51. Pia kuna mradi wa ujenzi wa runway na barabara kwa ujumla, wenye thamani ya zaidi ya bilioni 160, ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 85," amesema Mhe. Vuma.
Ameongeza kuwa, "Kamati tumeshuhudia wanasema kuona ni kuamini. Makaratasi peke yake hayatoshi kutufanya tusadiki yale tunayosemwa. Tumefika hapa, tumeshuhudia kazi kubwa inaendelea, na kweli yaliyosemwa yanaonekana kuwa yamefanyika. Tuna imani kuwa mradi huu ukikamilika kwa wakati utaweza kusaidia sana Watanzania, ambao wanausubiri kwa hamu kubwa sana," ameongeza.
Aidha, Mhe. Vuma amesema Kamati ya PIC inaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza mradi huo, ambao utachochea uchumi wa Dodoma kwa kuongeza safari nyingi za ndege kutoka mikoani na baadaye kwenda nje ya nchi.
Aidha, ameipongeza Wizara ya Ujenzi na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa usimamizi mzuri wa mradi huo, uzingatiaji wa thamani ya fedha, na ufanisi wa mradi, ikiwa ni pamoja na kuzingatia muda wa kukamilika kwa utekelezaji wa mradi huo.
Ametoa rai pia kwa TANROADS kuendelea kusimamia mradi huo ili ukamilike kwa asilimia 100 kwa ufanisi ndani ya muda uliopangwa kulingana na mkataba uliopo.
Naye, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa fedha za ujenzi wa kiwanja hicho, ambacho ni cha kimkakati na cha aina yake, kwani ni kiwanja kikubwa katika historia ya Tanzania tangu kupata uhuru—ambacho kimejengwa bila kurithiwa kutoka kwa wakoloni.
"Wataalamu wengi walioshiriki katika ujenzi wa kiwanja hiki ni Watanzania, pamoja na kuwa kampuni za ujenzi ni za Kichina. Hata hivyo, Watanzania wengi wamenufaika na wataendelea kunufaika. Sisi kama TANROADS tunaahidi kuendelea kusimamia kwa ukaribu ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa ufanisi," amesema Mhandisi Besta.
Toa Maoni Yako:
0 comments: