Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi amesema dhamira ya Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha nchi inaongozwa kwa kuzingatia misingi ya demokrasia na utawala bora na hivyo haipaswi kutiliwa shaka hata kidogo.

Balozi Nchimbi amesema katika utekelezaji wa dhana ya utawala bora, chini ya uongozi wa Rais Samia, Tanzania imeendelea kushuhudia kuwapo kwa uhuru wa mihimili mitatu ya dola, ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama.

Amesema mihimili hiyo ya dola imeendelea kutimiza wajibu wake kwa kufanya kazi vizuri na hivyo kuaminiwa na wananchi.

Balozi Nchimbi amesisitiza kuwa CCM chini ya Rais Samia, kitahakikisha dhamira hiyo pia inaendelezwa kwa vitendo kwa kuunga mkono uwapo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar kwa maslahi ya nchi na taifa kwani umoja huo ni zaidi ya vyama vya siasa.

Katibu Mkuu huyo wa CCM amesema hayo Jumanne, Machi 5, 2024, alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Marekani nchini, Michael Battle, kwenye Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar es Salaam, ambapo viongozi hao walijadiliana masuala anuai kuhusu ushirikiano na uhusiano wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili.

Katika mazungumzo yao, wamekubaliana nchi zote mbili kuangalia maeneo yanayoweza kuboreshwa kwa manufaa ya pande zote mbili hasa katika nyanja za biashara, uchumi na uwekezaji.

Vilevile, viongozi hao kwa pamoja wameelezea umuhimu wa kurahisishwa kwa upatikanaji viza.

“Ni wajibu wetu kuimarisha na kuuboresha uhusiano huu wa muda mrefu kama tulivyoupokea kutoka kwa waasisi na watangulizi wetu kama ulivyosema balozi. Tuuboreshe kwa ajili ya manufaa ya wananchi wetu wa pande zote mbili,'' anasema Balozi Nchimbi.

Naye Balozi Battle aliupongeza uongozi wa Rais Samia kwa jinsi ambavyo umekuwa wa wazi, imara na jasiri katika kusimamia misingi ya demokrasia na utawala bora.

“Kama unavyojua uhusiano huu ni wa muda mrefu, ukaboreshwa zaidi na urafiki uliokuwapo kati ya (Mwalimu) Nyerere na (John) Kennedy. Lakini pia kulikuwa na ukaribu kati ya (Jakaya) Kikwete na (George) Bush…na sasa tunaona ukaribu kati ya Rais Samia Suluhu Hassan na Makamu wa Rais (wa Marekani) Kamala Harris. Napenda kukuhakikishia na ujue kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Marekani ni mkubwa na halisi,” amesema Balozi Battle.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi akiwa kwenye mazungumzo na Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Mhe. Michael Battle, walipokutana Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar Es Salaam, kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu uhusiano kati ya Tanzania na Marekani, Machi 5, 2024.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: