Na Raymond Mtani BMH, Dodoma.
Imeelezwa kuwa Pombe na Sigara vyaweza kuwa miongoni mwa vyanzo vya Watoto kuzawaliwa na magonjwa yakiwemo magonjwa ya Moyo.

Hayo yamesemwa na Dkt. Victor Urio, Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, kwamba tafiti nyingi zinaonesha kati ya Watoto 1000 wanaozaliwa hai kote duniani 8 huwa na hitilafu mbalimbali za Moyo.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadilia kuwa zaidi ya Watoto 240,000 hufariki kwa magonjwa ya kuzaliwa nayo yakiwemo ya Moyo kila mwaka kabla ya kufikisha siku 28, huku zaidi ya 170,000 wakifariki kati ya umri wa mwezi 1 na miaka 5 kwa magonjwa hayo.

Kama hiyo haitoshi, WHO inatanabaisha Watoto 9 kati ya 10 wenye magonjwa ya kuzaliwa nayo wanatoka nchi za zenye Uchumi wa chini na wa kati, nchi za jumhiya ya Afrika Mashariki zikiwa miongoni mwa nchi hizo.

Dkt. Victor Urio, anasema takwimu hizo hazipingani na zinazoonekana katika kliniki ya Watoto ya Hospitali ya Benjamin Mkapa.

“Kwenye kila mwezi tunaona Watoto kati ya 10 hadi 20 wakiwa na magonjwa ya Moyo ya kuzaliwa nayo” Alisema Dkt. Urio.

Akiongeza kuwa kama ilivyo duniani kote Matundu na Mishipa ambayo haijafunga kwenye Moyo ni miongoni mwa hitilafu zinazowakabili Watoto wengi wanaobainika kuwa na Magonjwa ya Moyo ya kuzaliwa nayo Hospitalini hapo.

Ingawa, wataalamu hawajeweza kubaini sababu halisi za Watoto kuzaliwa wakiwa na hitilafu kwenye Moyo, yako mazingira yanayoongeza uwezekano wa mama kujifungua mtoto mwenye hitilafu za Moyo.

“Kutumia pombe na Kuvuta Sigara wakati wa Ujauzito, ni tabia zinaongeza uwezekano wa mama kujifungua mtoto mwenye hitilafu katika Moyo” Alisema Dkt. Urio.

Mbali na tabia hizo, kuchelewa kuanza Kliniki kwa mama mjamzito kunakomchelewesha kuanza matumizi ya vidonge vyenye madini ya Foliki humuweka mjamzito katika hatari ya kujifungua mtoto mwenye hitilafu ya Moyo.

“Vile vidonge vya Foliki vinahusika katika kujenga maumbile ya mtoto” alisema Dkt. Urio na kuongeza kuwa, ziko sababu za kurithi na za kimaumbile, na wakati mwingine maambukizi anayoyapata mama wakati wa ujauzito kama vile virusi vya Rubella yaweza kuwamweka katika hatari ya kujifungua mtoto mwenye hitlafu kwenye Moyo” Amesema Dkt. Urio

Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazopambana kuimarisha sekta ya Afya kwa kasi kubwa kwa kuhakikisha huduma za Afya zinapatikana jirani na mazingira wanayoishi wananchi wake, lakini vilevile kuboresha utoaji wa huduma kwa kupeleka wataalamu na vifaa tiba.

Kama haitoshi, serikali imeleta mfumo wa Bima ya Afya kwa wote, jambo litakaloleta unafuu wa gharama za matibabu.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: