Na Cathbert Kajuna - Kajunason Blog/MMG

Hanang', Katesh 27 Januari 2024: Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Cuthbert Sendiga mapema leo ameongoza zoezi la upandaji wa miti lililoendana na ukataji wa keki kwa ajili kusherekea miaka 64 ya kuzaliwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Akiongoza zoezi hilo la upandaji na kukata keki lililofanyika katika Shule ya Sekondari ya Katesh - Hanang, Mhe. Mkuu wa Mkoa amesema Miti zaidi ya 3,000 imepandwa katika maeneo yaliyoathiriwa na maporomoko ya tope, mawe na magogo ikiwa ni njia mojawapo ya kurejesha uoto wa asili uliopotea kufuatia uharibifu mkubwa wa mazingira uliosababishwa na mafuriko hayo yaliyotokea mwishoni mwa mwaka 2023. Kwa mwaka 2024, Mkoa wa Manyara umejipanga kupanda miti milioni 10.

Zoezi hilo lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mhe. Fredrick Sumaye Waziri Mkuu Mstaafu, Wakuu wa Wilaya wote wa Mkoa wa Manyara, Wakuu wa Taasisi Mbalimbali, Wakuu wa Idara pamoja, wananchi pamoja na watoto walioathirika katika maporomoko hayo.

Pamoja na hayo, Mkoa wa Manyara kwa kushirikiana na Wizara ya Afya umetekeleza zoezi la uhamasishaji wa mwezi wa saratani ya mlango wa kizazi, ambapo zaidi ya watu 328 katika Wilaya ya Hanang' wamejitokeza kufanya uchunguzi wa awali.

Aidha, elimu na hamasa inaendelea kutolewa kwa wananchi ili waweze kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu kwa wale watakaobainika kuwa na viashiria vya saratani.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: