Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohammed Mchengerwa
Na Shamimu Nyaki - WUSM, Dodoma
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohammed Mchengerwa amewaasa watanzania kulinda na kuhifadhi rasilimali na kumbukumbu ambazo ni ushahidi wa Harakati za Ukombozi wa Bara la Afrika katika maeneo waliyopo ambayo kumbukumbu hizo zinapatikana.
Katika taarifa aliyoitoa kwa Vyombo vya Habari leo Mei 25, 2022 jijini Dodoma, Mhe. Mchengerwa amesema Siku ya Afrika ambayo huazimishwa Mei 25 kila Mwaka,ni siku muhimu kwa waafrika wote ambapo kwa mwaka huu imebebwa na Kauli Mbiu isemayo "Urithi wa Ukombozi, Fahari ya Afrika na Kazi Iendelee".
"Kuthamini utanzania wetu ni jambo la msingi na ndiyo kielelezo na sifa iliyosababisha Umoja wa Afrika (AU) zamani (OAU) kuichagua Tanzania kuwa Makao Makuu ya Kamati ya Ukombozi wa Bara la Afrika na kuipa hadhi ya kuwa Mratibu wa Harakati za Ukombozi hadi nchi zote za Afrika zilipopata Uhuru mwaka 1994" amefafanua Mhe.Mchengerwa.
Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, ni wajibu wa jamii ya waafrika kuenzi kwa vitendo mashujaa wa Tanzania waliojitoa mhanga Kwa ajili ya Afrika chini ya Uongozi wa Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere.
Katika kuadhimisha siku hiyo, watanzania wameaswa kutembelea Ofisi ya Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Afrika ili kujifunza na kuona ushahidi waTanzania katika kuikomboa Afrika.
Toa Maoni Yako:
0 comments: