*Waridhishwa na Mradi wa ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama 
*Wapewa picha ya hali ya uboreshaji huduma za Mahakama

Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imetembelea Mradi wa Ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania ambapo imeonyesha kuridhishwa na Mradi huo na kuipongeza Mahakama kwa uboreshaji wa miundombinu ya majengo yake.

Akizungumza leo tarehe 24 Mei, 2022 mara baada ya ukaguzi wa Mradi huo unaojengwa katika eneo la ‘NCC Link’ mkoani Dodoma, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Daniel Sillo (MB) amesema kuwa Mahakama imepiga hatua kubwa katika uboreshaji wa huduma kwa lengo la kuwafikia wananchi.

“Kwanza nichukue fursa hii kwa niaba ya Kamati yetu ya Bunge ya Bajeti kumpongeza sana Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuridhia uboreshaji wa Mahakama hapa nchini, tumepita kwenye jengo la Kituo Jumuishi na vilevile tumekagua Mradi huu mkubwa ambao ni wa kihistoria kwa Afrika, na jengo ambalo linatajwa kuwa la sita kwa ukubwa (6) kati ya majengo ya Mahakama duniani, kwa kweli ni maboresho makubwa sana katika mustakabali wa kutoa haki,” amesema Mhe. Sillo.

Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa wao kama Kamati ya Bajeti wameridhishwa na matumizi ya fedha na mwenendo wa ujenzi wa Mradi huo na kusema kuwa ni wakati muafaka sasa kwa Wizara ya Katiba na Sheria kuendelea kuboresha taasisi nyingine zilizo chini ya mwamvuli wa Wizara hiyo ili waweze kwenda pamoja na kasi ya Mahakama.

Aidha, kabla ya kutembelea Mradi huo, Wajumbe hao walitembelea na kukagua jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Dodoma ambapo pamoja na ukaguzi walipata semina fupi iliyolenga kuwapa taswira ya hatua iliyofikiwa na Mahakama katika uboreshaji wa huduma zake.

Akizungumza wakati akiwasilisha Mada ya Utekelezaji wa Uboreshaji Huduma za Mahakama: Mafanikio na Changamoto, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amewajuza Wabunge hao kuwa safari ya uboreshaji wa huduma za Mahakama ni muhimu kwa kuwa umelenga katika kurahisisha upatikanaji wa huduma mahsusi ya Mahakama ya utoaji haki kwa wananchi.

Prof. Ole Gabriel amewahakikishia Wabunge hao kuwa Mahakama itaendelea kutunza rasilimali hizo ambazo Mahakama imeaminiwa na Serikali na kuahidi kuwa wataendelea kuwahudumia wananchi kwa weledi.

Wakichangia mada katika semina fupi iliyoandaliwa na Mahakama, Wajumbe wa Kamati hiyo akiwemo Makamo Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Omari Kigua (MB), Mhe. Dkt Charles Kimei (MB), Mhe. Shamsi Nahodha na wengine wameipongeza Mahakama na kuiomba Wizara ya Katiba na Sheria kuboresha pia Taasisi nyingine zilizo chini ya mwamvuli ili ziweze kwenda sambamba na kasi ya uboreshaji wa huduma za Mahakama.

Naye, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Geophrey Pinda amesema kuwa Wizara inaendelea na jitihada za kuboresha Taasisi za Sheria zilizo chini yake ili kwenda na kasi ya Mahakama hatimaye wananchi waweze kupata huduma ya haki bila vikwazo vyovyote.

Mradi wa Ujenzi wa jengo la Makao makuu ya Mahakama ambao umefikia asilimia 58 ya ujenzi wake utagharimu fedha za kitanzania shilingi 129,740,285,556.02 na unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 29 Desemba mwaka huu.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: