Mkurugenzi wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dk Amos Nungu akizungumza na wanahabari katika kongamano la waandishi wa habari kuhusu Wiki ya Ubunifu Tanzania 2022.
SERIKALI imesema haina lengo la kuwazuia wabunifu wadogo na kuficha kazi zao za kibunifu badala yake wanahakikisha usalama wa watu watakaotumia bunifu hizo.
Amesema itaendelea kuwatambua na kuwaendeleza wabunifu ambao wamejiajiri ili kutengeneza bidhaa za kurahisisha maisha ya watu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika kongamano la waandishi wa habari kuhusu Wiki ya Ubunifu Tanzania 2022, Mkurugenzi wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dk Amos Nungu amesema kuwa ubunifu umesaidia katika kutekeleza Mpango wa III wa maendeleo nchini na kwamba utasaidia vijana wengi kujiajiri.
Wiki ya ubunifu imeandaliwa na Mradi wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) kupitia mradi wa Funguo kwa kushirikiana na COSTECH, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na wadau wa sekta ya mawasiliano.
‘’Jukumu la serikali ni kulinda usalama wa watu wake. Kumekuwa na malalamiko mengi kuwa vijana wadogo wabunifu wamezuiwa kuendeleza kazi zao si kweli, kwa mfano kuna kijana kule Mbeya ambaye alibuni helikopta nilifika nikaiona lakini ni lazima tujihakikishie usalama wa abiria kama inaweza kuruka kulingana na viwango vya kimataifa na abiria watakuwa salama,’’ amesema Dk Nungu.
Amesema kuwa wabunifu wamefanikiwa kujiajiri na kuajiri watu wengine kwa kuuza bunifu zao na kuliingizia taifa fedha ambazo zinachangia katika ukuaji wa uchumi.
‘’Kutakuwa na Wiki ya Ubunifu ambayo itaanza Mei 16 hadi 20, mwaka huu katika Mikoa 16 ikiwemo Dar es Salaam, Dodoma, Zanzibar, Mbeya na Morogoro ili kuona kazi za kibunifu zilizofanywa na vijana wetu zitakazosaidia kutatua changamoto katika jamii,’’ alisisitiza.
Naye, Mtaalamu wa Miradi wa UNDP, Emmanuel Nnko amesema kuwa ubunifu ni nyenzo muhimu katika kusukuma maendeleo katika nyanja mbalimbali.
Amesema kuwa ulimwengu wa sasa umebadilika hivyo changamoto zilizopo haziwezi kutatuliwa kwa kutumia mbinu za zamani badala yake kwa njia ya ubunifu.
"Lengo letu ni kuweka jukwaa la wabunifu ili kuonesha bunifu zao zilizoleta utatuzi katika changamoto mbalimbali katika jamii ikiwemo sekta za maji, elimu, mazingira, fedha, kilimo, uvuvi na utalii," alisema Nnko.
Pia amesema kuwa wabunifu wanatumia bunifu zao kuhakikisha zinaleta ufanisi na kuchagiza maendeleo endelevu.
Amesema wapo wabunifu wengi mikoani ambao wanabuni vitu ambavyo vinajibu changamoto katika maeneo yao kwa kutumia teknolojia za kawaida.
"Tulipokea maombi zaidi ya 200 ambayo tulipata washindi 10 ambao tutawasaidia kukuza bunifu zao. Miongoni mwao ni waliobuni tochi kwa ajili ya kufukuza tembo na viboko wanaoharibu mazao shambani na waliobuni atamizi za kuangulia vifaranga kwa kutumia maganda ya mawese," alisisitiza.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya mitaji, UNCDF, Paul Damocha amesema kuwa watahakikisha wanaendelea kuwafadhili wabunifu kupata fedha na huduma za kitaalamu ili kuendeleza bunifu zao.
Amesema mfuko huo kwa kushirikiana na serikali wamekuwa wakitengeneza miongozo mbalimbali ya kuwasaidia wabunifu kuja na bunifu zitakazotoa majibu ya matatizo yaliyopo katika jamii na kuthibiti kazi hizo ili ziweze kuwa na manufaa.
‘’Tutahakikisha wabunifu wote ambao bunifu zao zimetambuliwa na serikali wanapatiwa fedha na msaada wa kitaalamu ili kukubuni vitu vingi zaidi na kuajiri watu wengine,’’ alisema Damocha.
Toa Maoni Yako:
0 comments: