Baadhi ya Wadau kutoka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali wakifuatilia Mkutano uliowakutanisha Jijini Dar Es Salaam kwa lengo la kupata ufumbuzi wa changamoto katika utoaji wa huduma za Afya nchini.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na wadau kutoka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa Sekta ya Afya mkoani Dar Es Salaam.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akizindua Mpango wa kudhibiti maambuzi ya Ugonjwa wa Korona kwa Mkoa wa Dar Es Salaam.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW
Na WAMJW - DSM
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amezindua Mpango Mkakati wa kudhibiti maambuzi ya Ugonjwa wa UVIKO-19 kwa Mkoa wa Dar es Salaam wenye lengo la kuthibiti kuenea kwa wimbi la nne la maambukizi hayo.
Dkt Gwajima amezindua Mpango huo leo Jiji Dar Es Salaam wakati wa Mkutano wa wadau wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa Sekta ya Afya.
Dkt Gwajima amesema kuwa Serikali imeendelea kuwekeza katika Sekta ya Afya kwa kuhakikisha huduma za Afya zinaboreshwa kwa kujenga miundombinu mbalimbali na kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma za Afya.
Ameongeza kuwa bado kuna changamoto katika kuhakikisha huduma za Afya zinatolewa katika ubora zikiwemo uhaba wa watumishi, vifaa tiba na miundombinu katika ujenzi na ukarabati ili kuimarisha utoaji wa huduma za Afya kwa Mkoa wa Dar Es Salaam na Tanzania nzima.
Aidha,Dkt. Gwajima ameeleza kuwa Mkutano huo uliowakutanisha wadau hao wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini kwa Sekta ya Afya utasaidia kutatua changamoto zilizopo katika utoaji wa huduma za Afya na yatatoa majibu na muelekeo katika kuhakikisha huduma bora za Afya zinapatikana.
Akielezea kuhusu wimbi la nne la maambukizi ya Ugonjwa wa UVIKO-19 amesema Wadau hao wasaidia katika kutoa elimu kawa wananchi katika kuhakikisha wanazingatia ushauri wa wataalam wa afya katika kujikinga na maambukizi ya Ugonjwa huo.
"Wadau mliopo hapa mtaona sehemu gani muhimu ya kusaidia hasa katika elimu kwa Umma ili wananchi waweze kujikinga na maambukizi hayo ambapo njia mbalimbali zinashauriwavkatika kujikinga na ugonjwa huu" alisema Dkt Gwajima.
Naye, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Dkt. Rashid Mfaume ameeleza kuwa Mkoa umejipanga katika kuhakikisha unapambana na maambukizi ya Ugonjwa wa UVIKO-19 kwa wimbi la nne na hasa kuhakikisha utoaji wa huduma za Afya katika vituo vya Afya vilivyopo mkoani humo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usajili na Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Grace Mbwilo amesema Ofisi ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali itaendelea kushirikiana na wadau hao kwa kusajili na kuratibu Mashirika hayo katika kuhakikisha yanasaidia na Serikali kutoa huduma kwa wananchi.
Mkoa wa Dar Es Salaam umekutanisha wadau kutoka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini kwa Sekta ya Afya kujadili na kuona namna ya kuboresha utoaji wa huduma za Afya mkoani hapo.
Toa Maoni Yako:
0 comments: