Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro amaeondoa zuio la usafirishaji bidhaa ghafi za misitu kwa masharti ikiwemo ‘veener’ na utomvu kutoka miti ya misindano kwenda nje ya nchi mpaka mwezi wa sita mwakani yaani 2022 na kuruhusu kontena 187 zilizopo bandari kusafirishwa na kontena zilizopo nje ya bandari zifuate utaratibu uliowekwa na Wizara ili zipate kibali cha kusafirishwa.

Akizungumza kwenye kikao kilichoratibiwa na Baraza la Biashara la Taifa (TNBC) Jijini Dar es Salaam, Dkt. Ndumbaro amesema lengo la Serikali ya Awamu ya Sita ni kuona sekta ya misitu inatoa mchango stahiki kwenye pato la taifa na kuwataka wadau kujiandaa na utekelezaji wa maazimio yaliyopitishwa kwenye kikao kilichowakutanisha wadau hao Novemba 15 mwaka huu Wilayani Mafinga.

“Malengo ya serikali ni kuona sekta ya misitu inaleta tija kwa wazalishaji wake. Nyinyi kama wadau hamna budi kujiandaa kutekeleza maagizo ya serikali ambayo na ndiyo maana nimetoa zuio nililoliweka ili mupate muda wa kujiandaa,’’ alisema Dkt. Ndumbaro.

Dkt. Ndumbaro alisisitiza kuwa, “Katika kipindi hiki cha mpito mpaka kufikia mwezi juni mwakani vibali vyote vitatolewa na Waziri kwa kufuata masharti yakiwemo kuleta taarifa za kodi, taarifa za haki za wafanyakazi, thamani halisi ya mzigo pamoja na kuwa na mpango kazi wa kampuni wa kuleta mashine haraka.

Aidha, Dkt.Ndumbaro aliwataka wafanyabiashara na watanzania kwa ujumla kukubaliana na mabadiliko ambayo ndiyo msingi wa maendeleo katika jamii yoyote duniani hivyo amehimiza jamii kuwa katika mtazamo chanya katika kupokea mabadiliko.

“Serikali imefanya tafiti na kujiridhisha kuwa faida inayopatikana katika kusafirisha malighafi ni ndogo hivyo ili kukuza kipato kupitia sekta ya misitu imeamua kuzuia usafirishaji wa mazao hayo na kuhimiza uwekazaji utakaotoa bidhaa ya mwisho na kwenda sokoni,’’ alisema Dkt.Ndumbaro.

Aliongezea kuwa serikali itaendelea kupaanua wigo na kutoa fursa zaidi za uwekezaji na ajira nchini kwani kwa kufanya zuio hilo kutachochea uwekezaji wa viwanda vikubwa hapa nchini jambo litakalozalisha ajira na kukuza pato la taifa.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa TNBC Dkt. Godwill Wanga mbali ya kumshukuru Waziri kwa kuja kuzungumza na wadau wa misitu, amewataka wadau hao kuwa na imani na serikali, kwani imefanya maboresho hayo ili sekta hiyo iwe na tija kwa wazalishaji na kuchangia kwenye pato la taifa.

“Kwa muda mrefu sasa sekta ya misitu imeonekana ikitoa mchango mdogo kwenye pato la taifa, kwa kuliona hilo serikali imekuja na maazimio haya ikiwa ni hatua ya kuifanya sekta hii iwe na tija sio tu kwa wazalishaji bali hata kwa uchumi wa nchi”, alisema Dkt. Wanga.

Dkt. Wanga aliongeza kuwa, “Sekta hii inahitaji tafiti nyingi ili wadau wajue fursa nyingi zaidi zilizopo, ambazo tukizutumia vyema itakuwa lulu kwa taifa.’’

Naye Mwenyekiti Mwenza wa kikundi kazi cha Misitu TNBC, Bw. Ben Sulus mbali ya kumpongeza Dkt. Ndumbaro kwa kutenga muda kuja kuwasikiliza wadau hao, amewataka wadau hao kubadilika na kuendana na matakwa ya serikali kwa kuwekeza zaidi kwenye kuleta mitambo na kuanzisha viwanda vingi nchini ili uzalishaji ufanyike hapahapa jambo ambalo litatengeneza fursa kubwa za ajira kwa watanzania.

“Sisi kama sekta binanfsi tujipange vizuri kwa kujiandaa kutekeleza kipindi hiki mpaka kufikia mwakani, tuweze kuanzisha viwanda vingi nchini vitakavyozalisha ajira kwa vijana wetu wengi zaidi”, alisema Bw. Sulus.

Waziri Dkt. Ndumbaro aliahidi kukutana tena na wadau wa sekta ya misitu tarehe 13 na 14 mwezi dssemba mwaka huu Jijini Arusha ili kuzungumza nao sambamba kuangalia namna utekelezaji wa maagizo ya serikali unavyofanyika.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: