Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti (kulia) akizindua maselo matatu mapya ya kulala mahabusu na wafungwa kwenye Gereza la Sumbawanga jana. Kushoto ni Mkuu wa Magereza Rukwa ACP Motrais Mwakilima
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti (katikati) akiwa na wajumbe wa Kamati ya Usalama Mkoa jana mara baada ya kuzindua mabweni matatu mapya ya kulala mahabusu na wafungwa Gereza Sumbawanga
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti (wa pili toka kulia) akiwa na Mkuu wa Gereza Sumbawanga SP Melkior Komba (kulia) na wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Sebastian Waryuba akifuatiwa na Mkuu wa Magereza Rukwa ACP Motrais Mwakilima jana mara baada ya uzinduzi wa masero ya kulala mahabusu Gereza Sumbawanga.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti ametoa wito kwa vyombo vya utoaji haki ikiwemo mahakama na Jeshi la Polisi kukamilisha kwa haraka upelelezi na utoaji haki kwenye kesi mbalimbali ili wasio na hatia waweze kuondolewa mahabusu hatua itakayosaidia kupunguza msongamano gerezani.
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Sebastian Waryuba akitoa salamu za wananchi kwenye uzinduzi wa masero ya kulala mahabusu kwenye Gereza Sumbawanga jana ambapo alitoa rai kwa wananchi kujiepusha na kufanya vitendo vitakavyopelekea wakutwe na hatia kisha kuwekwa mahabusu.(Habari na Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa)

Jeshi la Magereza Mkoa wa Rukwa katika kuadhimisha Miaka 60 ya Uhuru limefanikiwa kuzindua mabweni matatu mapya ya kulala wafungwa na mahabusu kwenye Gereza la Mahabusu Sumbawanga yakiwa na uwezo wa kulala watu Mia mbili (200).

Akizindua mabweni hayo 23.11.2021 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti amelipongeza Jeshi hilo kwa kuboresha mazingira ya kuhifadhi wafungwa na mahabusu hatua itakayopunguza msongamano.

“Gereza hili la mahabusu Sumbawanga lilianzishwa mwaka 1927 na wakoloni na hadi leo lilikuwa halijafanyiwa maboresho .Leo tukiwa kwenye shamrashara za maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru wa Taifa tunazindua mabweni haya hivyo ni furaha kuonesha tumepiga hatua kubwa za kimaendeleo” alisema Mkirikiti

Katika hatua nyingine Mkirikiti alitoa wito kwa vyombo vya utoaji haki ikiwemo mahakama na Jeshi la Polisi kuharakisha michakato ya upelelezi na usikilizwaji mashauri mahakamani ili watuhumiwa waweze kupata haki zao mapema hatua inayosaidia kupunguza msongamano magerezani.

“Vyombo vya kutoa haki vifanye kazi zake haraka na kwa uaminifu ili haki itendeke na wasio na hatia basi wasiendelee kukaa mahabusu bali waruhusiwe kurejea uraiani kuendelea na ujenzi wa Taifa” alisisitiza Mkuu huyo wa Mkoa wa Rukwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Gereza la mahabusu Sumbawanga Mrakibu wa Magereza ( SP) Melkior M. Komba alisema kukamilika kwa maselo (mabweni) hayo matatu kunaongeza uwezo wa kuhudumia mahabusu na wafungwa ambao kwa sasa wapo 422 huku uwezo uliokuwepo ni kuhudumia watu 200 pekee.

SP Komba alisema mabweni hayo maselo hayo matatu yatakuwa na uwezo wa kulaza mahabusu 200 kwa wakati mmoja hatua itakayosaidia kuondoa msongamano gerezani hapo.

Aliongeza kusema mradi huo wa maselo umegharimu shilingi Milioni 187 kati ya hizo shilingi Milioni 62 zilitolewa na Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP) Meja Jenerali Suleiman Mzee huku wadau wakichangia shilingi Milioni 124.

Aidha,SP Komba alisema kazi ya ujenzi wa mradi huo imefanikishwa na uwepo wa timu nzuri ya wataalam wa ujenzi ambao ni Askari na wafungwa hatua iliyosaidia kupunguza gharama za mradi huo ambazo awali zilikadiliwa kufikia shilingiilioni 256.

Kwa upande wake Mkuu wa Magereza Mkoa wa Rukwa Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Motrais Mwakilima akielezea mafanikio hayo ya Miaka 60 ya Uhuru alisema ni kutokana na jitihada za viongozi Wakuu wa Jeshi Waliopo sasa na wale ambao walipata nafasi huko nyuma kulitumikia Jeshi .

ACP Mwakilima aliongeza kusema kuwa Jeshi la Magereza linawashukuru wadau na wananchi wote kwa kuendelea kuliunga mkono hata kufanikisha Miradi yake ikiwemo ujenzi wa masero haya katika Gereza Sumbawanga.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Sumbawanga,Mkuu wa Wilaya hiyo Sebastian Waryuba alipongeza jitihada za kuboresha mahala pa kupumzika wafungwa na mahabusu lakini akatoa wito kwa wannachi kuepuka kujihusisha na vitendo vya kiuhalifu vitakavyopelekea wajikute wenye mikono ya vyombo vya dola.

“Kwa kuboresha mahala pa kulala wafungwa isiwe ni kigezo cha watu kukimbilia hapa bali tuendelee kuelimisha wananchi kuepuka vitendo vya kihalifu na uvunjifu wa amani ili wasifanye makosa yatakayopelekea kuwekwa mahabusu au kifungoni” alisema Waryuba.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: