Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania(TPDC) Mhandisi Kapuulya Musomba akifafanua jambo wakati anazungumzia Kongamano la Pili la sekta ya mafuta na gesi litakalofanyika Septemba 24 hadi 25 mwaka huu.
Kamishina Msaidizi wa Mendeleo ya Petroli kutoka Wizara ya Nishati akizungumza leo jijini Dar es Salaam kuhusu umuhimu wa Kongamano la pili la sekta ya mafuta na gesi
Mwanzilishi na Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Watoa Huduma za Mafuta na Gesi nchini Abdulsamad Abdulrahim akizungumza leo kuhusu Kongamano la Pili la Sekta ya Mafuta na Gesi ambalo litafanyika jijini Dar es Salaam Septemba 24 hadi 25.
Mwanzilishi na Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Watoa Huduma za Mafuta na Gesi akizungumza leo mbele ya waandishi wa habari kuhusu kongamano litakalofanyika Septemba 24 hadi 25 mwaka huu
*Ni kupitia Kongamano la pili la sekta ya mafuta, gesi litalokafanyika Septemba 24/25
Na Said Mwishehe, Globu ya jamii.
SERIKALI kupitia Waziri wa Nishati Dk.Medard Kalemani inatarajia kuzungumzia mwelekeo wa nchi katika kutumia nishati ya mafuta na gesi katika viwanda.
Waziri Kalemani atatoa muelekeo huo katika Kongamano la Pili la Sekta ya Mafuta na Gesi linalotarajia kufanyika kuanzia Septemba 24 hadi 25 mwaka huu jijini Dar es Salaam.Mbali ya Waziri kutoa mwelekeo, pia wadau muhimu wa sekta ya mafuta na gesi wakiwamo TPDC, PURA,EWURA, NEEC, ATOGS na TPSF watashiriki.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam kuhusu kongamano hilo Abdulsamad Abdulrahim kutoka Shirikisho la Watoa Huduma za Mafuta na Gesi nchini amesema Serikali na wadau wa sekta ya mafuta na gesi wameunga mkono na watashiriki kikamilifu.
Amefafanua kongamano hilo limeandaliwa na Pietro Fiorentini Tanzania kwa kushirikiana na CWC Group ambapo pamoja na mambo mengine mradi wa bomba la mafuta ghafi utachambuliwa wakati wa kongamano hilo.
“Mradi huo wa bomba la mafuta unatarajiwa kuleta fursa mbalimbali katika mnyororo wa thamani.Pia kongamano hili litajadili hatua za uendelezaji wa miradi ya gesi iliyopo nchini .
“Miradi ambayo itaifanya Tanzania kuwa mzalishaji na msambazaji mkubwa wa gesi katika ukanda wa Afrika Mashariki,”amefafanua.
Amesisitiza ikumbukwe sekta ya mafuta na gesi ina nafasi kubwa katika kuendeleza viwanda , kuchochea uchumi na kufungua fursa kwa watoa huduma waliopo nchini.
Abdulrahim amesema kupitia kongamano hilo fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi zitatambulishwa na kutangazwa.Hivyo kuwawezesha watoa huduma na kampuni zilizopo nchini kujenga ushirikiano wa kibiashara na kampuni za kimataifa.
Kuhusu mada ambazo zitajadiliwa ni gesi na mradi wa LNG na hasa katika taarifa muhimu na fursa.Pia kuweka mazingira ya kuvutia wawekezaji nchini, namna ya kuithaminisha gesi kama njia ya kuendeleza viwanda na kukuza uchumi.
Pia mjadala mwingine ni Nafasi kwa ajili ya bidhaa na huduma zilizopo nchini na fursa za ajira kwa ajili ya uendelezaji makini wa miradi ya mafuta na gesi Tanzania, Ushirikiano baina ya Serikali na wadau katika kuendeleza miradi iliyopo.
“Tunafahamu kuna mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda kuja Tanzania na umuhimu wa bomba Tanzania na katika ukanda wa Afrika Mashariki.Siku ya kongamano wadau watapata nafasi ya kuuliza maswali na
kupata majibu yake kuhusu mradi huo na mingine mikubwa inayoendelea ,”ameongeza.
Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Mhandisi Kapuulya Musomba pamoja na Kamishna Msaidizi wa Maendeleo ya Petroli kutoka Wizara ya Nishati Mhandisi Joyce Kisamo wamesema kongamano hilo ni muhimu na wanaamini litatoa fursa ya kujadiliwa kwa mambo muhimu yanayohusu mafuta na gesi.
Mhandisi Kisamo amesema kwamba ili kupima maendeleo ya nchi yoyote ile moja kipimo muhimu ni matumizi ya nishati , hivyo ni kongamano lenye tija kwa nchi yetu na hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Serikali ya Viwanda.
Ambapo amesema matumizi ya nishati ya gesi na mafuta yatatakiwa zaidi hasa katika kuendesha viwandani.
Toa Maoni Yako:
0 comments: