Na Mwandishi Wetu, Manyara.

MKUU wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, amepinga takwimu zinazoonesha kuwa upatikanaji wa huduma za dawa mkoani humo umefikia asilimia 93, akisema kuwa takwimu hizo haziakisi uhalisia wa hali iliyopo kutokana na wingi wa malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu ukosefu wa dawa na huduma muhimu za afya.

Sendiga ametoa kauli hiyo wakati wa kikao cha kuanza utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote (BAW) ngazi ya mkoa wa Manyara, kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, kikihusisha wadau wa afya wakiwemo Mganga Mkuu wa Mkoa, waganga wakuu wa wilaya pamoja na kamati za afya za halmashauri.

Amesisitiza kuwa utekelezaji wa bima ya afya kwa wote hauwezi kufanikiwa endapo wananchi wataendelea kukumbana na kero za ukosefu wa dawa, vipimo na huduma nyingine muhimu katika vituo vya afya na hospitali. “Huduma bora za afya lazima ziende sambamba na bima ya afya kwa wote. Wananchi hawapaswi kulalamika,” amesema RC Sendiga.

Katika kuhakikisha mpango huo unafanikiwa, Mkuu huyo wa Mkoa amezielekeza halmashauri zote za Manyara kuhakikisha zinafikisha elimu ya Bima ya Afya kwa Wote hadi ngazi ya kaya, kwa kuwafikia wananchi wa makundi yote wakiwemo vijana wa bodaboda, bajaji, wazee na kaya masikini, ili waweze kuelewa faida na umuhimu wa kujiunga na bima hiyo.

Aidha, amewataka waganga wafawidhi chini ya usimamizi wa Mganga Mkuu wa Mkoa na waganga wakuu wa wilaya kuhakikisha huduma zote muhimu, ikiwemo dawa na vipimo, zinapatikana kwa wakati katika hospitali na vituo vya kutolea huduma za afya, ili kuondoa malalamiko na kurejesha imani ya wananchi.

Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ulianza rasmi Januari 26, 2026, ukiwa na lengo la kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya kwa uhakika, nafuu na kwa usawa, hatua ambayo Mkoa wa Manyara umeanza kuitekeleza kikamilifu kwa kuhamasisha wananchi na kusimamia ubora wa huduma za afya.

Na WMJJWM – Dodoma

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, ametambuliwa rasmi kuwa miongoni mwa Wanawake 100 Wanaoheshimiwa wa Asili ya Afrika kwa mwaka 2026, kutokana na mchango wake mkubwa katika uongozi na maendeleo ya kijamii nchini na barani Afrika kwa ujumla.

Tuzo hiyo hutolewa na Kongamano la Wanawake wa Afrika (Africa Women Summit) kama heshima maalum kwa wanawake waliodhihirisha uongozi wa kipekee, uadilifu wa hali ya juu na mchango chanya katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa. Orodha hiyo inalenga kuenzi wanawake wanaovunja vikwazo, kubadilisha simulizi za maendeleo na kuhamasisha kizazi kijacho cha viongozi wanawake.

Katika toleo la mwaka 2026, wanawake mashuhuri kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika wametambuliwa, huku Tanzania ikiwakilishwa na Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, kutokana na juhudi zake katika kuendeleza usawa wa kijinsia, uwezeshaji wa wanawake, ulinzi wa watoto na ujumuishaji wa makundi maalum katika mipango ya maendeleo ya taifa.

Akizungumza baada ya kutambuliwa, Dkt. Gwajima amesema heshima hiyo ameipokea kwa shukrani kubwa, akimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa kinara wa uwezeshaji wa wanawake duniani na kwa kuendelea kuwaamini na kuwapa nafasi wanawake kushika nafasi za uongozi. Amesema utambuzi huo ni matokeo ya imani na malezi ya kiuongozi aliyopata chini ya Rais Samia.

Dkt. Gwajima ameahidi kuendelea kuchochea utekelezaji wa falsafa ya Kazi na Utu kwa kujituma na kuhakikisha huduma na programu za wizara yake zinawafikia wananchi wote, hususan wanawake, watoto na makundi yenye mahitaji maalum, ili kuenzi heshima hiyo na kutimiza maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa muda wake katika uongozi, Dkt. Gwajima amekuwa mstari wa mbele katika kuongoza mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, kuimarisha ulinzi wa mtoto, kukuza usawa wa kijinsia na kuhakikisha makundi maalum yanajumuishwa kikamilifu katika mipango na fursa za maendeleo, hatua zilizomjengea heshima kubwa ndani na nje ya nchi.

Na Mwandishi Wetu, Iringa

MKUU wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James (Pichani), ameonesha kukerwa na kitendo cha Mkuu wa Shule moja mkoani humo aliyerudisha nyumbani wanafunzi waliochelewa kuleta rimu baada ya shule kufunguliwa, akisema hatua hiyo imekosa hekima, busara na haizingatii ustawi wa watoto.

Akizungumza kuhusu hali ya lishe na upatikanaji wa chakula kwa wanafunzi shuleni, RC Kheri James amesema viongozi na watumishi wa umma wana wajibu wa kutumia busara katika kufanya maamuzi, hasa yale yanayohusu moja kwa moja haki na maisha ya watoto. Amesisitiza kuwa maamuzi yanayowagusa wanafunzi yanapaswa kufanywa kwa kuzingatia mazingira halisi ya jamii.

RC Kheri ameongeza kuwa si wazazi na walezi wote wana uwezo sawa wa kiuchumi, hivyo ni muhimu kwa viongozi wa shule kuelewa changamoto zinazowakabili baadhi ya familia kabla ya kuchukua hatua zinazoweza kuwaumiza watoto. “Hatuwezi kudhani kila mzazi ana uwezo sawa. Maisha ya watu yanatofautiana, na hili lazima litambuliwe,” amesema.

Aidha, amewataka viongozi wa elimu kuacha tabia ya kujisahau na badala yake waweke mbele maslahi ya wanafunzi, akisisitiza kuwa elimu ni haki ya msingi kwa kila mtoto na changamoto ndogo za vifaa vya shule hazipaswi kuwa sababu ya kuwanyima watoto haki hiyo.

Amehitimisha kwa kutoa wito kwa walimu wakuu na wasimamizi wa shule zote mkoani Iringa kuhakikisha wanajenga mazingira rafiki ya ujifunzaji, yanayochochea ushiriki wa wanafunzi wote bila ubaguzi, kwa lengo la kufanikisha maendeleo ya elimu na ustawi wa watoto.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akicheza pamoja na kikundi cha ngoma za asili cha Wanafunzi wa Shule ya Msingi Kisutu mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), tarehe 29 Januari, 2026.



Vatican City — Tanzania has reaffirmed its long-standing diplomatic and moral partnership with the Holy See, emphasizing shared commitments to peace, dialogue, human dignity, and social development.

The message was delivered by the Minister for Foreign Affairs and East African Cooperation, Hon. Mahmoud Thabit Kombo (MP), during an official audience with Pope Leo XIV at the Vatican on 29 October 2025. Minister Kombo conveyed warm greetings and a special message from President Samia Suluhu Hassan, underscoring Tanzania’s appreciation for the Catholic Church’s contribution to education, healthcare, social welfare, and national cohesion.
He praised the Church’s moral leadership and its role in promoting unity and peaceful coexistence in Tanzania, noting that its institutions continue to complement government efforts, particularly among vulnerable communities.

Tanzania also welcomed the Holy See’s proposal to establish a resident diplomatic mission at the Vatican, describing the move as an important step toward strengthening structured cooperation. Currently, Tanzania is represented by a non-resident ambassador based in Berlin.

During discussions, Minister Kombo briefed the Pope on Tanzania’s commitment to national reconciliation following post-election tensions, guided by President Samia’s 4R philosophy — Reconciliation, Resilience, Reforms, and Rebuilding. He highlighted ongoing efforts, including inclusive dialogue and the establishment of an independent review process to promote accountability and prevent future unrest.

Pope Leo XIV welcomed Tanzania’s approach and expressed his readiness to continue praying for peace, unity, and stability in the country. He also recalled his pastoral experiences in Tanzania, saying they left a lasting impression and strengthened his personal connection to the nation.

In addition to the Papal audience, Minister Kombo held talks with senior Vatican officials, including Archbishop Paul Richard Gallagher, focusing on deepening diplomatic cooperation and collaboration in social development.

The Ministry of Foreign Affairs said the engagement reflects Tanzania’s diplomatic direction of being “non-aligned but multi-engaged,” pursuing partnerships that advance national unity, peace, and shared prosperity.

Na Mwandishi Wetu, Njombe.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe limekanusha vikali taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii zikidai kuwa askari wa polisi mkoani humo alichomwa moto na kuporwa silaha, likizitaja taarifa hizo kuwa za uongo, za kupotosha na zisizo na ukweli wowote.

Akizungumza na vyombo vya habari Januari 28, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Mahamoud Banga, amesema hakuna tukio la aina hiyo lililotokea katika mkoa huo na kwamba taarifa zinazosambazwa ni za uzushi mtupu.

“Tunakanusha kuwepo kwa tukio hilo. Hakuna askari aliyekumbwa na tukio la kuchomwa moto wala kuporwa silaha mkoani Njombe. Taarifa hizi ni za uongo na zinapotosha jamii,” amesema ACP Banga.

Kamanda huyo ameonya kuwa watu wanaojihusisha na kutengeneza, kusambaza au kushiriki kusambaza taarifa za uongo kupitia mitandao ya kijamii wanakiuka sheria za nchi na maadili ya jamii, na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

“Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi wanaoandaa na kusambaza taarifa za uongo kuacha mara moja tabia hiyo, kwani ni kinyume cha sheria na haina manufaa yoyote kwao, familia zao wala kwa jamii kwa ujumla,” ameongeza.

Aidha, Polisi wameeleza kuwa wanaendelea kuwafuatilia watu waliotumia picha mjongeo (video) ya tukio la zamani lililohusisha askari waliokuwa wakitoa msaada kwa wananchi, na kuliwasilisha kama tukio jipya kwa lengo la kupotosha umma.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe pia limehakikishia wananchi kuwa linaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kulinda usalama wa raia na mali zao kwa kushirikiana na wananchi kupitia programu ya Polisi Jamii, sambamba na kufanya doria, misako na operesheni mbalimbali katika maeneo tofauti ya mkoa huo.

Mwisho, Polisi wamewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola na kuhakikisha wanapata taarifa sahihi kutoka kwenye vyanzo rasmi kabla ya kuzisambaza.

Na Mwandishi Wetu – Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Madini imezidi kuonesha dhamira yake ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uwekezaji wa kimkakati barani Afrika, baada ya kukaribisha rasmi kampuni kutoka Korea Kusini kuja kuwekeza katika sekta ya madini nchini.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, amesema uwekezaji huo unahitajika zaidi katika maeneo ya utafiti wa madini, uongezaji thamani, pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa katika uchimbaji na uchakataji wa madini, hususan madini muhimu na ya kimkakati.
Mbibo ametoa kauli hiyo Januari 28, 2026 jijini Dodoma, wakati wa kikao kati ya Wizara ya Madini na ujumbe kutoka Korea Kusini uliowakilisha Shirika la Kukuza Biashara na Uwekezaji la Korea (KOTRA) pamoja na Kampuni ya HD Construction Equipment, inayojihusisha na utengenezaji wa mitambo na teknolojia za uchimbaji madini.

Amesema maboresho ya sera na sheria yaliyofanywa na Serikali yamelenga kuvutia wawekezaji wenye mtaji, teknolojia na nia ya kuwekeza kwa muda mrefu, hasa katika ujenzi wa viwanda vya kuchakata madini ndani ya nchi na uhamishaji wa teknolojia kwa Watanzania.

“Tanzania iko tayari kwa ubia wa kimkakati unaoongeza ajira, mapato ya ndani na ushindani wa kimataifa. Tunakaribisha wawekezaji wanaoleta suluhisho za kisasa kwenye mnyororo mzima wa thamani wa madini, kuanzia utafiti hadi uongezaji thamani ndani ya nchi,” amesema Mbibo.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi na Kamishna wa Biashara wa KOTRA Ofisi ya Dar es Salaam, Kim Sangwoo, amesema Korea Kusini ina dhamira ya kuongeza uwekezaji wake katika Ukanda wa Afrika Mashariki kupitia miradi yenye tija na uwajibikaji, huku Tanzania ikitajwa kuwa miongoni mwa nchi zenye mazingira rafiki ya uwekezaji.

Naye Meneja Mkuu wa Kampuni ya HD Construction Equipment, Soohong Min, amesema kampuni za Korea zina uzoefu mkubwa katika teknolojia za kisasa za uchimbaji, mitambo mizito, pamoja na mifumo bora ya uzalishaji, ambayo inaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ajenda ya Tanzania ya uongezaji thamani wa madini.
● Majadiliano kati ya pande hizo mbili yalihusisha maeneo muhimu kama:

● Utafiti wa kina wa madini kwa kutumia teknolojia za kisasa

● Uchakataji na uongezaji thamani wa madini

● Ujenzi wa viwanda na miundombinu ya uzalishaji

● Uhamishaji wa teknolojia kwa wataalamu wa ndani

Kwa pamoja, pande zote zimeonesha dhamira ya kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kiteknolojia, huku Serikali ikisisitiza kuwa mlango uko wazi kwa wawekezaji wanaoendana na dira ya maendeleo jumuishi na endelevu ya Taifa.

KOTRA ni taasisi ya Serikali ya Korea Kusini iliyoanzishwa mwaka 1962 kwa lengo la kukuza biashara ya kimataifa na uwekezaji wa kigeni, na ina ofisi katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania kupitia ofisi yake ya Dar es Salaam.
 Na Mwandishi Wetu – Dodoma

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imezindua rasmi mfumo mpya wa huduma kwa wateja unaotumia teknolojia ya akili unde (Artificial Intelligence) ujulikanao kwa jina la BWANABOOM, unaolenga kurahisisha na kuharakisha upatikanaji wa huduma kwa wadau wa elimu nchini kwa saa 24 kila siku.

Uzinduzi wa mfumo huo umefanyika leo Januari 28, 2026 katika ofisi za Makao Makuu ya HESLB jijini Dodoma, ukihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na wadau wa sekta ya elimu.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (WyEST), Profesa Daniel Mushi, ambaye ameipongeza HESLB kwa kuendelea kuwa kinara katika matumizi ya teknolojia za kisasa kuboresha huduma kwa wananchi.

“Leo tunaongeza huduma ya akili unde ‘BWANABOOM’ kama njia nyingine muhimu ya kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wadau wa elimu. Hili ni jambo la kujivunia na linapaswa kuigwa na taasisi nyingine nchini,” amesema Prof. Mushi.

Amesema mfumo huo ni hatua muhimu katika safari ya mageuzi ya kidijitali kwenye sekta ya elimu, na kusisitiza umuhimu wa HESLB kuendelea kuuboresha ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia duniani.

Aidha, Prof. Mushi ametoa wito kwa HESLB kuzingatia kwa makini masuala ya usalama wa taarifa binafsi za watumiaji, kupima kiwango cha kuridhika kwa wateja mara kwa mara, pamoja na kuangalia uwezekano wa kuanzisha huduma za lugha ya ishara kidijitali ili kuwahudumia wadau wenye ulemavu wa kusikia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, amesema BWANABOOM ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa taasisi hiyo wa kutumia teknolojia za kisasa ili kuongeza ufanisi, uwazi na urahisi wa upatikanaji wa huduma kwa wanafunzi na wadau wengine wa elimu.

“Tunataka kuhakikisha huduma za HESLB zinawafikia wadau kwa urahisi zaidi, kwa wakati na kwa gharama nafuu kupitia majukwaa ya kidijitali,” amesema Dkt. Kiwia.

Naye Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Bi. Jaqueline Humbaro, amepongeza ubunifu huo na kuahidi kuwa balozi wa mfumo huo miongoni mwa wanafunzi ili wahakikishe wanatumia ipasavyo fursa hiyo mpya.

BWANABOOM unapatikana kupitia tovuti rasmi ya HESLB (www.heslb.go.tz) na pia ndani ya akaunti za wanafunzi kwenye mfumo wa SIPA, na unatarajiwa kupunguza gharama za usafiri, kuokoa muda, na kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.

Uzinduzi wa mfumo huo unaonesha dhamira ya dhati ya HESLB katika kutumia teknolojia ya akili unde kama nyenzo ya kuleta mageuzi chanya katika maendeleo ya elimu nchini.