Articles by "HABARI"
Showing posts with label HABARI. Show all posts

NA MWANDISHI WETU

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, imetembelea miradi mbalimbali mkoani Njombe leo tarehe 09 Januari, 2025.

Kamati hiyo imetembelea kituo cha Afya cha Njombe Mjini kilichopo katika Halmashauri ya mji wa Njombe kwa lengo la kujionea huduma zinazotolewa katika kituo hicho ikiwemo huduma za upimaji UKIMWI, pamoja na kutembelea Shirika lisilo la kiserikali "COCODA" linalohudumia watu wanaishi na virusi vya UKIMWI.

Kamati hiyo imeongozwa na Mhe. Dr. Elibariki Kingu Mwenyekiti wa kamati na Mbunge wa Singida Magharibi, akiambatana na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anaeshughulikia Masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mheshimiwa Ummy Nderiananga



Aidha kamati imepokea taarifa ya mambukizi ya UKIMWI mkoani Njombe, ambapo mkoa una watu 66,979 wanaishi na Virusi vya UKIMWI huku jitihada mbalimbali zikiendelea kufanyika ikiwa ni pamoja na ugwaji wa kondom.

Hata hivyo kamati imetoa pongezi kwa Mkoa wa Njombe, kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Asasi zinazojihusisha na suala la kuhakikisha maambukizi ya VVU, yanapungua Mkoani Njombe.

Pamoja na hayo, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga, ametoa shukrani kwa kamati ya kudumu ya Bunge, huku akiahidi Serikali kuendelea kushirikiana na wadau kwani bado kuna changamoto kubwa ya maambukizi ya VVU kwa vijana.

MTOTO REGNALDO SAMWELI MSUYA MIAKA (16) ANATAFUTWA, INADAIWA ALIONDOKA NYUMBANI KWAO 15/12/2024 HADI SASA HAJULIKANI ALIPO.
NYUMBANI KWAO NI KINONDONI MTAA MWANANYAMALA KWA KOPA, DAR ES SALAAM. ANASOMA SHULE YA SECONDARY MAKUMBUSHO KIDATO CHA TATU. KWA YOYOTE ATAKAYE MUONA TUNAOMBA ATOE TAARIFA KWENYE KITUO CHOCHOTE CHA POLISI KILICHO KARIBU.

TAARIFA NAMBA YA POLISI NI MWJ/RB/1893/2024 AU KWA SIMU NAMBA HII 0782 136333
Dar es Salaam. Tarehe 7 Januari 2025: Katika kuukaribisha mwaka mpya 2025, Benki ya CRDB imezindua mikopo ya ada kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini kote. Mikopo hiyo inayoitwa Ada Fasta ni mwendelezo wa juhudi za Benki ya CRDB kukidhi mahitaji na matarajio ya wateja wake ili kuwawezesha kukabiliana na changamoto za kifedha wanakokabiliana nazo.


Akizindua mikopo hiyo inayotolewa kupitia Programu ya SimBanking, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo amesema kila mzazi au mlezi mwenye uhitaji anaweza kupata mkopo huo ili kumruhusu mwanafunzi kuendelea na masomo kulingana na ratiba ya muhula husika.

“Mteja anaweza kukopa mpaka shilingi milioni 3 ambazo atazirudisha ndani ya miezi sita. Riba ya mkopo huu ni asilimia 13 tu mwaka, gharama ndogo zaidi ukilinganisha riba iliyopo sokoni. Nawakaribisha wazazi wote kuitumia fursa hii kuhakikisha watoto wetu wanasoma bila tatizo lolote la ada,” amesema Nshekanabo.

Mkurugenzi huyo amesema wameizindua huduma hiyo kipindi hiki wakitambua kuwa Januari ni mwezi wenye changamoto nyingi za kifedha zinazotokana na mahitaji makubwa yanayokuwepo ikiwamo ada za wanafunzi, kodi ya nyumba na mahitaji mengine muhimu hasa baada ya kila mtu kuwa ametumia kiasi kikubwa cha fedha kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka.


Ikiwa Benki inayomsikiliza mteja na kumweka mbele katika mikakati ya biashara, amesema wakati wote wanabuni huduma na bidhaa zinazokidhi mahitaji ya wateja na Januari hii wamekuja na jambo jipya mahususi kwa kila mzazi au mlezi wa mwanafunzi nchini.
Zaidi ya muongo mmoja Benki ya CRDB ilizindua nakuutambulisha Mfumo wa Makusanyo ya Ada Shuleni yaani School Fees Management System ambao mpaka sasa unatumiwa na zaidi ya shule 1,000 nchini kote ambazo sasa wanafunzi wake watanufaika na mikopo hii iliyozinduliwa.


“Hii ni fursa kwa shule zote binafsi nchini kujiunga na mfumo huu wa makusanyo ya ada ii kutoa fursa kwa wazazi kukopa ada wakati wowote watakapohitaji ili watoto waendelee na masomo yao. Wazazi wote waliopo kwenye shule zinazoutumia mfumo huu wawe ni wateja wetu ama la, wanayo fursa ya kunufaika na mikopo hii,” amesema Nshekanabo.

Mzazi au mlezi atakayeomba mkopo huu, amesema atapata fedha husika zitakazoingizwa kwenye akaunti ya shule moja kwa moja na yeye kupata risiti ya uthibitisho kwamba amelipa ada inayotakiwa kwa ajili ya mtoto wake.

Kwa kuwawezesha wazazi na walezi kulipa ada kwa wakati, Nshekanabo amesema wana imani watakuwa wamesaidia kuboresha elimu kwa kuwawezesha wanafunzi kuhudhuria masomo yao bila vikwazo huku shule zikiweza kujiendesha na kutoa maarifa bora yanayohitajika kwa watoto wa Kitanzania.

Kwa mzazi au mlezi ambaye ameajiriwa na mshahara wake unapitia Benki ya CRDB, anaweza kupata mkopo wa ada kwa kuingia kwenye Programu ya SimBanking kisha akabofya sehemu ya mikopo ambako atatakiwa kuingiza ‘control number’ aliyotumiwa na shule kwa ajili ya malipo ya ada na programu itamwonyesha kiasi cha juu anachoruhusiwa kukopa.
Baada ya hapo, mteja atatakiwa kuingiza kiasi anachokitaka na kupendekeza muda anaotaka kulipa deni hilo ndani ya miezi sita ili kukamilisha maombi yake. Akishafanya hivyo, Benki ya CRDB itaingiza fedha zilizoombwa kwenye akaunti ya shule anakosoma mtoto hivyo kumruhusu asome kwa utulivu.

Ukiacha faida zilizopo kwa pande zote mbili yaani shule na mzazi au mlezi, mfumo wa makusanyo ya ada wa Benki ya CRDB ni rahisi kuutumia kwani mteja anaweza kulipa ada kupitia SimBanking, CRDB Wakala au kutembelea tawi la Benki ya CRDB.

Vilevile, mteja anaweza kulipa ada ya mwanafunzi kupitia M-pesa, Tigopesa, Airtel Money au Halopesa bila kulazimika kupeleka risiti ya malipo shuleni kwani taarifa huwa zinafika huko moja kwa moja. Kwa upande wa shule, faida iliyopo ni kwamba inakusanya ada kwa wakati na kupata taarifa papo hapo.
Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya CRDB, Stephen Adili akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Mikopo ya ada kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini kote (Ada Loan) iliyozinduliwa na Benki ya CRDB ili kukidhi mahitaji na matarajio ya wateja wake kwa kuwawezesha mkopo ili kukabiliana na changamoto za kifedha hasa katika kipindi hiki cha mwanzo wa mwaka. Uzinduzi huo umefanyika leo kwenye ukumbi wa Benki hiyo, jijini Dar es salaam leo.

Rais wa Chama cha Wawekezaji Binafsi katika Elimu nchini (TAPIE), Mahmod Mringo akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Mikopo ya ada kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini kote (Ada Loan) iliyozinduliwa na Benki ya CRDB ili kukidhi mahitaji na matarajio ya wateja wake kwa kuwawezesha mkopo ili kukabiliana na changamoto za kifedha hasa katika kipindi hiki cha mwanzo wa mwaka. Uzinduzi huo umefanyika leo kwenye ukumbi wa Benki hiyo, jijini Dar es salaam leo.


Afisa bima wa VodaBima kutoka Vodacom Tanzania PLC kanda ya Ziwa, Hellen Masali akimuwekea mafuta mteja wa kampuni hiyo Omari Ramadhan jijini Mwanza. Mafuta hayo yametolewa bure ikiwa ni moja ya adhma ya kampeni yao ya msimu wa sikukuu ya kurejesha tabasamu kwa wateja wake katika msimu huu wa sikukuu. Ili kushinda Mafuta bure endelea kulipia kwa kutumia M-pesa.
Afisa bima wa VodaBima kutoka Vodacom Tanzania PLC kanda ya Ziwa, Hellen Masali akimuwekea mafuta mteja wa kampuni hiyo Zacharia Regan jijini Mwanza.
Mkuu wa kanda ya ziwa kutoka Vodacom Tanzania PLC, Venance Chapaulinge akimuwekea mafuta mteja wa kampuni hiyo Rajabu Kawambwa jijini Mwanza.
Mkuu wa kanda ya ziwa kutoka Vodacom Tanzania PLC, Venance Chapaulinge akimuwekea mafuta mteja wa kampuni hiyo Rajabu Kawambwa jijini Mwanza.

NaMwandishi Wetu,
Manyara


Waziri wa nchi Ofisi ya Rais ,Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo amepengeza Wawekezaji wazawa wa kiwanda cha Mati Super brands limited kwa kulipa kodi stahiki za serikali na kutengeneza ajira kwa vijana hivyo kuchochea maendeleo ya Mkoa wa Manyara na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza mara baada ya kutembelea kiwanda cha Mati Super Brands limited ,waziri kitila mkumbo amepongeza wawekezaji hao waliowekeza ambao wamelipa kodi ya kiasi cha shilingi bilioni 8 kwa mwaka 2024 na kuchangia maendeleo ya nchi.

“Rais Dr.Samia Suluhu Hassan anapambana kuongeza ajira kwa vijana wa Kitanzania na Mati Super Brands Limited imeajiri Watanzania 269 hilo ni jambo kubwa” Anaeleza Profesa Kitila Mkumbo ,Waziri wa nchi Ofisi ya Rais ,Mipango na Uwekezaji
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Mati Super Brands Limited David Mulokozi amesema kuwa kiwanda hicho kimekua na mchango katika jamii na kimekua kikilipa kodi stahiki za serikali ikiwemo kondi ya Ongezeko la thamani (VAT) ,ushuru wa uzalishaji wa bidhaa,kodi ya mapato (income tax Pamoja na kodi nyingine.

“Kwa kipindi cha miaka mitatu tumekua tukilipa kodi ambapo mwaka 2022 tumelipa kodi bilioni 7,2023 tumelipa bilioni 7.9 ,mwaka 2024 tumelipa kodi bilioni 8 na mwaka 2025 tunatarajia kulipa kodi zaidi ya bilioni 12” Anaeleza Mkurugenzi wa Kampuni ya Mati Super Brands Limited ,David Mulokozi
Katika kuufunga mwaka 2024 kwa huduma bora, Benki ya CRDB imefungua matawi mapya mawili mkoani Mara yaliyopo Mugango katika Wilaya ya Musoma Vijijini na Sirari wilayani Tarime.

Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa amesema uzinduzi wa matawi hayo ni sehemu ya jitihada za Benki kuiishi kaulimbiu yake ya ‘ulipo, tupo’ kwa kuwafuata wananchi katika kila pembe ya nchi na kuwapa huduma bora za fedha kwa maendeleo yao binafsi na kuchangia uchumi wa taifa pia.
“Mkoa wa Mara una shughuli nyingi za kiuchumi kuanzia migodi mikubwa na machimbo ya madini, uvuvi, kilimo na biashara ya mpakani hivyo ni muhimu kuwa na huduma za uhakika za fedha ili kuwajumuisha wananchi kwengi katika uchumi. Ulikuwa ni mpango wa Benki yetu ya CRDB kuhakikisha tunafungua matawi haya mawili kabla mwaka 2024 haujaisha,” anasema Raballa.


Kabla ya ufunguzi wa matawi hayo mapya, Raballa amesema wananchi wa maeneo hayo walikuwa wanapata huduma za benki kupitia kwa mawakala waliotapakaa maeneo tofauti. Kwa mkoa mzima wa Mara, amesema Benki ya CRDB inao zaidi ya mawakala 600 wakiwamo 195 wanaohudumia katika Wilaya Ya Tarime na 35 Musoma Vijijini.
“Kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya wateja wilayani Tarime na Musoma, Benki yetu iliona kuna umuhimu wa kuboresha huduma ili kuendana na mahitaji yaliyopo sasa na yatakayojitokeza baadaye. Tulifanya utafiti wa kina kabla ya kujenga matawi haya yatakayowahudumia wananchi wa Mugango na Sirari pamoja na maeneo jirani,” amesema Raballa.


Kutokana na uzinduzi wa matawi hayo mawili, Benki ya CRDB sasa imefikisha jumla ya matawi 10 mkoani Mara ambayo ni Musoma, Tarime, Bunda, Serengeti, Nyamongo, Rorya, Shirati, Mugango na Sirari hivyo kuifanya kuwa na mtandao mpana zaidi wa matawi nchini kuliko benki nyingine yoyote nchini.
Akifungua tawi la Sirari, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mheshimiwa Meja Edward Flowin Gowele amesema huduma za fedha ndio msingi wa maendeleo ya mwananchi binafsi, kaya na taifa kwa ujumla hivyo kilichobaki ni umakini wa wananchi kubuni miradi itakayowainua kiuchumi kwa kuzikabili changamoto zilizopo kwenye maeneo yao ili kunufaika na fursa zinazojitokeza.

“Tawi hili ni sehemu salama kwa wananchi kuhifadhi akiba zenu za fedha. Ni mahali ambapo wafanyabiashara mtapata mikopo ya kuimarisha miradi yenu na wafanyakazi nao wataweza kutimiza malengo yao. Benki ni rafiki wa kila mwananchi anayewa na kupanga maendeleo yake, tulitumie tawi hili kujinufaisha kwa kujenga uchumi imara wa kila mmoja wetu,” amesema Mheshimiwa Gowele.

Licha ya kunufaika na mikopo inayotolewa, Mheshimiwa Gowele amewahimiza wananchi wa Sirari, Wilaya ya Tarime, Mkoa wa Mara na Tanzania nzima kwa ujumla kuwekeza kwenye Hatifungani ya Samia Infrastructure Bond inayoendelea kuuzwa na Benki ya CRDB ili kupata fedha zitakazowezesha ujenzi wa barabara zilizo chini ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).
“Ukiwekeza katika hatifungani hii una uhakika wa kupata faida ya asilimia 12 inayotolewa kila mwaka kwa muda wote wa miaka mitano wa uhai wake. Lakini, kumiliki hatifungani hii ni sawa na kuwa na nyumba, unaweza kuitumia kama dhamana kuchukua mkopo kutoka taasisi yoyote ya fedha. Nawasihi kila mmoja wenu na Watanzania wote kwa ujumla, kuitumia fursa hii kuwekeza kwenye hatifungani hii,” amesisitiza Mheshimiwa Gowele.

Kwenye uzinduzi wa tawi la Mugango, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gerald Musabila Kusaya amesema ni fursa kwa wananchi wa Musoma kunufaika na huduma zinazotolewa na Benki ya CRDB zikiwamo zilizo chini ya Programu ya Imbeju inayolenga kuwawezesha vijana na wanawake.
“Ufunguzi wa tawi hili umesogeza kwa karibu fursa za Programu ya Imbeju. Nawaomba wajasiriamali mlitumie tawi hili kupata mitaji wezeshi itakayosaidia kuinua biashara zenu. Hapa, mtapata ushauri wa kitaalamu ia wa namna bora ya kukuza shughuli zenu kwa maendeleo binafsi na taifa pia,” amesema Kusaya.

Sambamba na ufunguzi wa tawi la Benki ya CRDB Sirari, Benki ya CRDB imekabidhi madawati 50 yenye thamani ya shilingi milioni 5 kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kujifunzi kwa wanafunzi wa Wilaya ya Tarime. Madawati hayo yamepokelewa na Mheshimiwa Gowele aliyesema yatasaidia kupunguza uhaba uliopo katika shule za msingi na sekondai wilayani Tarime.

Na WMJJWM-Dar es Salaam.

Jamii imehimizwa kuwakumbuka watu wenye Mahitaji Maalum katika msimu huu wa Sikukuu kwa kuwapatia zawadi na mahitaji mbalimbali ili waweze kusheherekea kwa furaha Sikukuu za mwisho wa mwaka.

Rai hiyo imetolewa Desemba 25, 2024 na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake Jinsia na Wanawake na Makundi Maalum, (anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii na Makundi Maalum) Wakili Amon Mpanju wakati akikabidhi zawadi mbalimbali kwa watoto wanaolelewa katika Makao ya Taifa ya Watoto Kurasini Dar Es Salaam, kwa niaba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

"Msimu wa Sikukuu jamii inapaswa kuwakumbuka na kuwasaidia watu wenye mahitaji Maalum kama wezee na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi ni jambo la baraka na linatoa matumani Kwaao na kujiona ni kama watu wengine" amesema Wakili Mpanju.

Aidha Wakili Mpanju ametoa wito kwa Mashirika, Taasisi za Serikali, Mashirika yasiyo ya Kiserikali na jamii kuhakikisha watoto, wazee na watu wenye mahitaji Maalum wanasherehekea kwa furaha Sikukuu za mwisho wa mwaka kwa kuwakumbuka kwa zawadi na mahitaji mbalimbali ya kibinadam.

Kwa upande wake Makamu Mfawidhi wa Makao hayo Farida Ismael amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa zawadi hizo ambazo zitawasaidia watoto kula na kunywa na kufurahia sikukuu za mwisho mwaka kama watoto wengine.

Naye mmoja wa mtoto anayelelewa katika Makao hayo Festo Elias kwa niaba ya watoto wenzake amemshukuru Rais Samia kwa kuwakumbuka watoto katika kipindi hiki cha Sikukuu na ameeleza kufurahia zawadi hizo na kuomba wadau na taasisi zingine kufanya hivyo mara kwa mara.