Na Mwandishi Wetu, Mombasa
Mwananchi wa Kisauni, Yusuf Garare, ameweka historia mpya baada ya kuvunja rekodi ya dunia ya Guinness kwa kuchoma nyama (barbecue) kwa muda mrefu zaidi duniani, akifikisha saa 87, dakika 10 na sekunde 30 bila kukoma.
Tukio hilo la kihistoria limefanyika katika eneo la Kisauni, Mombasa, likishuhudiwa na mamia ya wananchi, wadau wa chakula na wageni kutoka sehemu mbalimbali za Pwani ya Kenya, waliokusanyika kushuhudia safari hiyo ya kipekee.
Hadi kufikia muda huo, Garare alikuwa ameweka rekodi mpya ya “Longest Barbecue Marathon (Individual)”, akiipiku rekodi ya awali iliyoshikiliwa na mpishi kutoka nchi nyingine.
Akizungumza baada ya kumaliza zoezi hilo la zaidi ya siku nne mfululizo, Garare alieleza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya maombi, nidhamu na ushirikiano mkubwa kutoka kwa jamii ya Kisauni na wafuasi wake kote nchini.“Nilijituma kwa moyo wote nikijua kwamba hii siyo tu kuhusu mimi, bali ni kuhusu Pwani na vijana wote wa Afrika Mashariki. Nimefanya hili kuonyesha kuwa tukiamua, tunaweza kufikia viwango vya dunia,” alisema Garare kwa furaha.
Kwa sasa, matokeo hayo yanatarajiwa kuthibitishwa rasmi na Guinness World Records, baada ya kupitia ushahidi wote wa muda, video na mashahidi wa tukio hilo.
Wakazi wa Mombasa na maeneo jirani wameelezea fahari yao kwa Garare, wakisema amekuwa mfano wa kuigwa kwa vijana wanaotafuta mafanikio kupitia juhudi na ubunifu.
“Huu ni ushindi wa Pwani, ushindi wa Kenya na ushindi wa Afrika Mashariki,” alisema mmoja wa mashabiki wake.
Tukio hilo limeendelea kuwa gumzo katika mitandao ya kijamii, ambapo watu wengi wanampongeza Garare kwa kuonyesha moyo wa kujituma, uvumilivu na kujenga imani mpya kwa kizazi kipya cha vijana wajasiriamali.


.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments: