Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Katibu wa Bunge, Baraka I. Leonard, amewataka wabunge wote wateule kufika Dodoma kuanzia Novemba 8 hadi 10, 2025 kwa ajili ya usajili na maandalizi ya kikao cha kwanza cha Bunge la Kumi na Tatu, kitakachofanyika Novemba 11, 2025.
Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa tarehe 5 Novemba 2025, kikao hicho kitajumuisha shughuli mbalimbali ikiwemo kusomwa kwa tangazo la Rais la kuitisha Bunge, uchaguzi wa Spika na Naibu Spika, kiapo cha uaminifu kwa wabunge wote, pamoja na uteuzi wa Waziri Mkuu.
Aidha, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atazindua rasmi Bunge jipya katika hafla itakayofanyika siku hiyo hiyo ya Novemba 11.
Wabunge wote wateule wametakiwa kufika wakiwa wamevaa mavazi rasmi na kuwasilisha nyaraka muhimu kama vile hati za kuchaguliwa, vitambulisho vya taifa, namba za akaunti za benki, vyeti vya ndoa (kwa walioo ama kuolewa), vyeti vya kuzaliwa kwa watoto walio chini ya miaka 21, vyeti vya elimu pamoja na wasifu binafsi (CV).
Kwa mujibu wa tangazo hilo, uchaguzi wa Spika na Naibu Spika utafanyika kujaza nafasi zilizotangazwa katika tangazo la Serikali Na. 1482A na 1482B la tarehe 4 Novemba 2025.



Toa Maoni Yako:
0 comments: