Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amekabidhiwa rasmi Ofisi ya Makamu wa Rais kutoka kwa mtangulizi wake, Dkt. Philip Mpango, katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, Novemba 4, 2025.

Katika tukio hilo, Dkt. Nchimbi alimshukuru na kumpongeza Dkt. Mpango kwa mchango mkubwa alioutoa wakati wa kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kipindi cha kwanza cha Serikali ya Awamu ya Sita.

Akizungumza baada ya makabidhiano hayo, Makamu wa Rais Dkt. Nchimbi alisema atahakikisha anatekeleza kwa ufanisi majukumu aliyopewa kwa uwezo wake wote, kwa lengo la kuendelea kusaidia juhudi za Rais Samia katika kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuwaletea Watanzania maendeleo endelevu.

Dkt. Nchimbi aliongeza kuwa ataendeleza kazi nzuri iliyoanzishwa na mtangulizi wake, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi za Serikali katika kuimarisha huduma kwa wananchi.

“Ofisi hii imefanya kazi kubwa katika kipindi cha kwanza cha Awamu ya Sita, jambo lililorahisisha utekelezaji wa majukumu ya Serikali na maandalizi ya kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025,” alisema Dkt. Nchimbi.

Aidha, alimshukuru Dkt. Mpango kwa utumishi wake uliotukuka na kumtaka kuendelea kutoa mchango wake pale utakapohitajika, hasa katika utekelezaji wa sera za uchumi wa buluu na masuala mengine ya kitaifa.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais Mstaafu Dkt. Philip Mpango alimpongeza Dkt. Nchimbi kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo muhimu, akimtaka atekeleze majukumu yake kwa hekima, unyenyekevu na kwa maslahi ya wananchi wote.

“Ushauri wangu ni kuwa na moyo wa uvumilivu, busara na kujituma katika utumishi wa umma, kwani nafasi hii ni ya kumsaidia Rais katika majukumu makubwa ya kuliongoza taifa,” alisema Dkt. Mpango.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, watumishi wa umma na wawakilishi wa taasisi za kitaifa.

Imetolewa na:
Ofisi ya Makamu wa Rais
Dodoma, Novemba 4, 2025
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: