Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameongoza Kikao Maalumu cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (CC) kilichofanyika leo Jumatano, Novemba 5, 2025, jijini Dodoma.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka Ofisi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, kikao hicho kilijadili masuala mbalimbali ya kisera na kiutendaji, pamoja na kufanya uteuzi wa wagombea wa nafasi za Spika na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sambamba na uteuzi wa wagombea wa nafasi hizo katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar.


Kikao hicho kinafuatia maandalizi ya kikao cha kwanza cha Bunge la Kumi na Tatu, kinachotarajiwa kufanyika jijini Dodoma wiki ijayo, ambapo wabunge wateule wataapishwa na baadaye kufanyika kwa uchaguzi wa viongozi wa juu wa Bunge.

Aidha, ndani ya kikao hicho, Dkt. Samia aliwahimiza wajumbe wa Kamati Kuu kuendelea kudumisha misingi ya chama, umoja, na nidhamu ya kisiasa, akisisitiza umuhimu wa kuweka mbele maslahi ya wananchi na taifa.

“CCM itaendelea kusimama kidete katika kuhakikisha uongozi unaozingatia haki, umoja na maendeleo ya Watanzania wote,” alinukuliwa akisema Dkt. Samia wakati wa kikao hicho.
Kamati Kuu ni chombo cha juu cha maamuzi ndani ya Chama Cha Mapinduzi, chenye wajibu wa kupanga mikakati ya kisiasa na kiutawala kabla ya maamuzi rasmi ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).

Kikao hicho cha leo kimekuwa miongoni mwa vikao muhimu vinavyoashiria mwanzo wa mwelekeo mpya wa uongozi wa Bunge jipya, huku Watanzania wakisubiri kwa hamu majina ya wagombea walioteuliwa kuwania nafasi hizo za juu za uongozi.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: