Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini (CCM), Mhe. Daniel Baran Sillo, amechaguliwa kwa kishindo kuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika uchaguzi uliofanyika leo Alhamisi, Novemba 13, 2025, mjini Dodoma.

Uchaguzi huo umefanyika muda mfupi baada ya Bunge kumthibitisha Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kufuatia uteuzi uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Katika uchaguzi huo, Mhe. Sillo amepata kura 371 za ndiyo kati ya kura 371 zilizopigwa, ikiwa ni ushindi wa asilimia 100, jambo lililoonyesha imani kubwa ya wabunge kwa uongozi wake.

Baada ya kutangazwa mshindi, Mhe. Sillo alikula kiapo cha uaminifu na kuahidi kushirikiana kwa karibu na Spika wa Bunge pamoja na wabunge wote katika kuhakikisha Bunge linafanya kazi kwa ufanisi, weledi na kwa maslahi ya Taifa.

“Ninaahidi kufanya kazi kwa ushirikiano, nidhamu na uwazi mkubwa. Nitahakikisha Bunge linaendelea kuwa jukwaa la mijadala yenye tija kwa wananchi,” alisema Mhe. Sillo baada ya kula kiapo.

Naibu Spika huyo mpya anatarajiwa kuzungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuahirishwa kwa kikao cha Bunge, katika lango kuu la kuingilia bungeni.

Kabla ya kuchaguliwa kushika wadhifa huo, Mhe. Sillo amekuwa mbunge anayejipambanua kwa utendaji na ushiriki wake katika mijadala mbalimbali bungeni, huku akitambulika kama kiongozi kijana mwenye msimamo na uwajibikaji mkubwa.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: