Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeidhinisha rasmi uteuzi wa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu kuwa Waziri Mkuu mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kufuatia uteuzi uliotangazwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Katika kikao cha Bunge kilichofanyika leo Alhamisi, Novemba 13, 2025, wabunge walimpigia kura Dkt. Mwigulu na kumpitisha kwa kishindo, baada ya kupata kura 369 za ndiyo kati ya kura 371, huku kura mbili zikiharibika.

Dkt. Mwigulu, ambaye alikuwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa miaka mitano ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Sita, ameeleza dhamira yake ya kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha maono na ahadi za Rais Samia yanatekelezwa kwa ufanisi kwa ajili ya ustawi wa Watanzania.

“Watumishi wa umma wavivu, wazembe, wala rushwa na wenye lugha mbaya kwa Watanzania — tuwe tayari. Nitakuja na fekeo na rato. Maono ya Rais lazima yatekelezwe,” alisema Dkt. Mwigulu katika hotuba yake ya shukrani bungeni, huku akipongezwa kwa kauli yake ya ujasiri.

Aidha, aliwataka Watanzania kumtanguliza Mungu, kudumisha amani, na kusisitiza kuwa Serikali yake itasikiliza na kuheshimu sauti za wananchi wote, wakiwemo wabunge wa upinzani.

Kuapishwa Ikulu Kesho Ikulu, Chamwino

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais – Ikulu, kupitia Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dkt. Moses Kusiluka, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, atamuapisha Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kesho Ijumaa, Novemba 14, 2025, saa 4:00 asubuhi katika Ikulu Chamwino, Dodoma.

Taarifa hiyo, iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Bi. Sharifa B. Nyanga, imeeleza kuwa hafla hiyo itahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Bunge na vyombo vya ulinzi na usalama.

SAFARI YA UONGOZI

Dkt. Mwigulu, ambaye anatambulika kama mfano wa mafanikio yanayotokana na bidii na kujituma, alikulia katika familia yenye maisha ya kawaida kijijini, ambako aliwahi kuchunga ng’ombe akiwa mtoto. Ameeleza mara kadhaa kuwa maisha hayo yalimjenga katika nidhamu, uvumilivu na kuthamini kazi halali.

Kisiasa, alianza kama Naibu Waziri wa Fedha chini ya Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete, kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi (2015), kisha Waziri wa Mambo ya Ndani (2016), na hatimaye Waziri wa Fedha (2021–2025).

Kwa sasa, Dkt. Mwigulu anaingia rasmi katika ukurasa mpya wa uongozi kama Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiahidi kuongoza kwa uadilifu, nidhamu na uzalendo.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: