Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, amemteua Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Taarifa hiyo imetangazwa leo, Novemba 13, 2025, ambapo jina la Dkt. Mwigulu, ambaye ni Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), limewasilishwa rasmi bungeni jijini Dodoma kwa ajili ya kupigiwa kura ya kumthibitisha na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wabunge wanatarajiwa kupiga kura muda mfupi ujao kuthibitisha uteuzi huo kabla ya kula kiapo cha wadhifa huo mkubwa wa kitaifa.

Dkt. Mwigulu, ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwemo Waziri wa Fedha na Mipango pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, anatajwa kuwa miongoni mwa viongozi vijana waliopitia ngazi nyingi za uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wadadisi wa siasa wanasema uteuzi huo unaonesha dhamira ya Rais Samia kuendelea kuimarisha uongozi wa serikali yake kwa kuwapa nafasi viongozi wenye uzoefu, nidhamu na ufanisi katika utumishi wa umma.

Baada ya kuthibitishwa na Bunge, Dkt. Mwigulu atachukua rasmi nafasi ya Waziri Mkuu na kuanza majukumu yake mara moja.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: