Nairobi, Oktoba 16, 2025: Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini Kenya (KCAA) imetangaza kufungwa kwa muda kwa shughuli zote katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kufuatia kuwasili kwa mwili wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Amolo Odinga.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa KCAA, Emile N. Arao, imeeleza kuwa idadi kubwa ya waombolezaji waliingia maeneo yaliyopigwa marufuku ndani ya uwanja huo, hali iliyolazimu kufanyika kwa kufungwa kwa tahadhari ili kuruhusu vikosi vya usalama kurejesha utulivu na kuhakikisha usalama.

“Wananchi na wasafiri wanashauriwa kubaki watulivu na kuepuka maeneo ya uwanja wa ndege hadi taarifa mpya itakapotolewa. Shughuli za kawaida zitarejeshwa mara tu uwanja utakapohakikishwa kuwa salama katika kipindi cha saa mbili zijazo,” ilieleza sehemu ya taarifa ya KCAA.

Mamlaka hiyo imesema kuwa tayari imetoa taarifa rasmi kwa mashirika yote ya ndege (NOTAM) kuhusu kusimamishwa kwa shughuli hizo kwa muda mfupi.

Mwili wa Odinga, ambaye alifariki dunia Oktoba 15 nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu, umeletwa nchini leo na umepokelewa kwa heshima kubwa na viongozi wa serikali, familia na mamia ya waombolezaji waliokusanyika uwanjani hapo.

Rais wa Kenya, William Ruto, tayari ametangaza siku saba za maombolezo ya kitaifa na maandalizi ya mazishi ya kitaifa kwa heshima ya Odinga yanaendelea kuratibiwa.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: