
Na Mwandishi Wetu, Nairobi
Shughuli za kawaida katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) zimeanza tena baada ya kusimamishwa kwa muda kufuatia vurugu zilizozuka wakati wa mapokezi ya mwili wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Amolo Odinga, Alhamisi asubuhi.
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Kenya (KAA) ilithibitisha kurejea kwa shughuli zote za ndege na kuwahakikishia abiria na umma kuwa usalama umeimarishwa.
“JKIA sasa imefunguliwa kwa shughuli za kawaida baada ya kusimamishwa kwa muda leo asubuhi. Tunawashukuru abiria, mashirika ya ndege na wananchi kwa subira na ushirikiano wao,” alisema Kaimu Mkurugenzi Mkuu na Mtendaji wa KAA, Mohamud Gedi.
Awali, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Kenya (KCAA) ilitangaza kusimamishwa kwa muda kwa shughuli zote za ndege kutokana na hali ya usalama iliyoibuka baada ya mamia ya waombolezaji na waendesha bodaboda kuvamia eneo la mapokezi la State Pavilion walipokuwa wakiusubiri mwili wa marehemu Raila.
Hali hiyo ilisababisha kuvunjika kwa taratibu za mapokezi rasmi, ambapo baadhi ya waombolezaji walivunja vizuizi, kupenya kwenye maeneo yaliyokuwa yamezuiwa, na hata wengine kuruka kuta za uzio huku wakipiga kelele za kumsifu Odinga na kubeba matawi ya miti.
Kufuatia purukushani hizo, vikosi vya usalama vilivyohusisha wanajeshi na GSU vililazimika kuimarisha doria na kuwatawanya waombolezaji kabla ya kurejesha hali ya utulivu.
Licha ya taharuki hiyo, hali ilibaki ya amani huku waombolezaji wakiimba nyimbo na kauli mbiu za kisiasa zinazohusiana na marehemu kiongozi huyo. Baada ya utulivu kurejea, mwili wa Raila ulipelekwa katika Lee Funeral Home jijini Nairobi kabla ya kupelekwa Kasarani kwa ajili ya kuonyeshwa hadharani.
KAA imewataka abiria waliokuwa na safari wakati wa kusitishwa kwa muda kwa shughuli hizo kuwasiliana na mashirika yao ya ndege kwa taarifa mpya za ratiba za usafiri.


Toa Maoni Yako:
0 comments: