Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza ratiba ya uchaguzi wa marudio wa udiwani katika Kata ya Nyakasungwa, Jimbo la Buchosa, Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa mkoani Mwanza, kufuatia kifo cha aliyekuwa mgombea wa CCM, Ndugu Feruzi Rajabu Kamizula, kilichotokea Oktoba 9, 2025.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Oktoba 18, 2025 na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Bw. Kailima R. K., tume ilisitisha shughuli zote za uchaguzi kuanzia Oktoba 10, ikiwemo kampeni, na sasa imetoa ratiba mpya ya kufanyika kwa uchaguzi huo.

Kwa mujibu wa NEC, fomu za uteuzi kwa mgombea wa udiwani kupitia CCM zitatolewa kuanzia Oktoba 18 hadi 24, 2025, na uteuzi rasmi wa mgombea utafanyika Oktoba 24, 2025.

Kampeni za uchaguzi zitaanza Oktoba 25 hadi Oktoba 28, 2025, na kusimama kuanzia Oktoba 29 hadi Novemba 1, ili kupisha siku ya kupiga kura na kutangazwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Kampeni zitaendelea tena kuanzia Novemba 2 hadi Desemba 29, 2025.

Siku ya kupiga kura kwa uchaguzi wa marudio katika Kata ya Nyakasungwa imepangwa kufanyika Jumanne, Desemba 30, 2025.

Tume imeeleza kuwa uteuzi mpya hautahusisha mgombea mwingine yeyote aliyechaguliwa kihalali kabla ya kusitishwa kwa uchaguzi, isipokuwa kama atajitoa rasmi. Aidha, imezikumbusha chama husika na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia Katiba, Sheria na taratibu za uchaguzi ili kuhakikisha mchakato unafanyika kwa amani na haki.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: